Iran: Nchi za Kiarabu zitafakari matatizo ya Waislamu badala ya uchochezi
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeitaka Jumuiya ya nchi za Kiarabu isitisishe uchochezi dhidi ya Iran na badala yake itafakari matatizo ya umma wa Kiislamu.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Bahram Qasemi katika kujibu matamshi yasiyofaa dhidi ya Iran yaliyotolewa na Ahmad Abul Gheit Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu, amemnasihi atathmini utendaji wa jumuiya hiyo siku zilizopita na kujiepusha na uchochezi kuhusu matatizo ya eneo na ulimwengu wa Kiislamu. Bahram Qasemi amesema katika hali ambayo moja ya malengo ya kuasisiwa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu ni kutatua migogoro baina ya nchi wanachama kwa njia za amani, jumuiya hiyo inasaidia nchi moja ya Kiarabu kuishambulia nchi nyigine ya Kiarabu na ndugu kumuua ndugu. Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kukaririwa madai yasiyo na msingi na uhasama hakutabadili ukweli wa mambo katika eneo. Amesema kuna udharura kwa umma wa Kiislamu kuwa na msimamo mmoja katika kukabiliana na adui wa pamoja ambaye ni utawala ghasibu wa Israel na magaidi wakufurishaji. Hivi karibuni Ahmad Abu Gheit Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya nchi za Kiarbau alitoa matamshi yasiyo na msingi kuwa eti Iran inaingilia mambo ya ndani ya nchi za Kiarabu.