Dec 07, 2023 03:33 UTC
  • Iran: Israel inawajihiwa na siku za kutisha kutokana na majibu makali ya muqawama

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema wanamapambano wa makundi ya muqawama ya Palestina wameendelea kutoa majibu makali na ya nguvu kwa uvamizi wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza, na kwamba mwenendo wa majibu hayo utauweka utawala wa Kizayuni kwenye hali mbaya katika siku zijazo.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo usiku wa kuamkia leo katika mazungumzo ya simu na mwenzake wa Qatar, Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al Thani na kuongeza kuwa, "Muqawama wa Kiislamu mpaka sasa umetoa majibu ya nguvu kwa vitendo vya kivamizi vya utawala wa Israel, na kwa mwenendo huu, siku zijazo zitakuwa mbaya mno kwa utawala huo."

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amelaani vikali jinai za utawala haramu wa Israel dhidi ya wanawake na watoto wadogo katika Ukanda wa Gaza, ambao ndio wahanga wakuu wa mashambulizi ya kutisha ya utawala huo pandikizi.

Amir-Abdollahian amebainisha kuwa, kitendo cha utawala wa Kizayuni kuanza tena jinai zake za kivita dhidi ya watu wa Gaza kinaonyesha kupuuza na kukaidi kwake matakwa ya jamii ya kimataifa na sheria za kimataifa.

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Qatar sanjari na kulaani hatua ya Israel ya kuanzisha upya vita dhidi ya wakazi wa Gaza, wameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kusimamisha mauaji ya kimbari na jinai hizo za kivita katika eneo hilo lililo chini ya mzingiro.

Majibu ya muqawama kwa chokochoko za Israel Gaza

Kadhalika wawili hao wamesisitizia haja ya kusimamishwa mashambulizi ya Israel dhidi ya Gaza, kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu, na kuongezwa misaada ya kibinadamu katika eneo hilo; miito iliyotolewa na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Israel ilianzisha tena kampeni ya kijeshi Ijumaa iliyopita kufuatia kumalizika muda wa usitishaji vita, ambapo mpaka sasa imeua shahidi Wapalestina zaidi ya 16,000 tangu ianzishe vita dhidi ya Gaza mnamo Oktoba 7, kufuatia operesheni iliyofanywa na harakati za muqawama za eneo hilo katika hatua ya kulipiza kisasi kufuatia jinai za miongo kadhaa za utawala huo dhidi ya Wapalestina.

 

Tags