Wairani 23,000 wasio na hatia wameuawa shahidi kwa vitendo vya kigaidi
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu wa Idara ya Mahakama ya Iran amekumbusha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa mhanga mkubwa zaidi wa vitendo vya magaidi na kubainisha kwamba: hadi sasa watu elfu 23 wasio na hatia wameuawa shahidi kutokana na vitendo vya kigaidi.
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama ya Iran amegusia ulazima wa kuwatetea waathirika, kutekeleza uadilifu na kukabiliana na mwenendo wa kutochukuliwa hatua vitendo vya magaidi wa MKO na akaongeza kuwa: hatua zote hizo ni miongoni mwa misingi ya kupambana na ugaidi na kuboresha haki za binadamu.
Kuhusu kusikilizwa kesi ya genge la kigaidi la MKO, Gharib Abadi amesema: lengo la kuendeshwa kesi hiyo ni kutekeleza uadilifu; na hatua za kisheria na kimahakama lazima zichukuliwe ili kukabiliana na vitendo vya megenge ya kigaidi, kwa sababu yanatumia chaka la hatua za kisiasa kuficha jinai zao za kigaidi na kuzifanya zionekane kuwa ni harakati za kutetea haki za binadamu; kwa hivyo ni lazima hatua zao zifichuliwe.
Katibu wa Tume ya Haki za Binadamu ya Idara ya Mahakama ya Iran aidha amesema: ushahidi na nyaraka za jinai zinazofanywa na makundi ya kigaidi inapasa zikabidhiwe kwa nchi na jumuiya za kimataifa, na suala hilo ni miongoni mwa malengo muhimu ya kuendeshwa kesi hiyo.
Halikadhalika, Gharib Abadi amesisitiza ulazima wa kutumia uwezo wa kisheria na mahakama kwa ajili ya kuyapandisha kizimbani makundi ya kigaidi na akatilia mkazo pia kutekelezwa hukumu zitakazotolewa.
Wanachama 104 wa genge la kigaidi la Munafikiana (MKO) watashtakiwa katika mahakama ya jinai ya mkoa wa Tehran, na mahakama hiyo imewataka wanachama waliotoroka wa kundi hilo kuwasilisha mahakamani mawakili wao wa kisheria.
Genge la kigaidi la MKO ndilo lililohusika na mauaji ya Wairani zaidi ya elfu 17.../