Iran yazionya Marekani na Uingereza: Msijaribu kuzipima ghadhabu za mataifa ya eneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian amelaani vitendo vya uchokozi vya hivi karibuni dhidi ya nchi za Asia Magharibi na kuzionya Marekani na Uingereza kwamba zisijaribu kuzipima ghadhabu za mataifa ya eneo hili.
Kamandi Kuu ya Marekani (CENTCOM) ilisema katika taarifa siku ya Ijumaa kwamba vikosi vyake vilishambulia zaidi ya sehemu 85 "kwa ndege kadhaa" wakati wa uvamizi wa usiku ziliofanya katika maeneo ya Iraq na Syria.
Vyombo vya habari vya serikali ya Syria viliripoti kuwa uvamizi huo wa Marekani ulilenga maeneo kadhaa katika mkoa wa mashariki wa Dayr al-Zawr na mji wa Bukamal karibu na mpaka wa Iraq, lakini havikutoa maelezo kuhusu kiwango cha uharibifu na idadi kamili ya waliouawa.
Kwa mujibu wa ofisi ya Waziri Mkuu wa Iraq Muhammad Shia' al-Sudani, watu 16 waliuawa miongoni mwao wakiwamo raia na 25 walijeruhiwa katika mashambulizi ya anga yaliyofanywa na Marekani nchini humo.
Katika hatua nyingine tena ya hujuma na uvamizi dhidi ya ardhi ya Yemen, Marekani na Uingereza usiku wa manane wa kuamkia jana zilifanya mashambulizi kadhaa ya anga kwenye mikoa ya Sana'a, Hudaydah na Sa'ada, mbali na mengine kadhaa.
Pentagon ilidai kuwa mashambulizi hayo yalilenga maeneo 13 ndani ya Yemen na kugonga vituo vya kuhifadhia silaha, mifumo ya makombora na ya urushiaji ambayo Vikosi vya Majeshi ya Yemen na harakati ya wananchi ya Ansarullah vinaitumia kushambulia meli za utawala wa Kizayuni wa Israel katika Bahari Nyekundu kuwaunga mkono Wapalestina katika Ukanda wa Gaza.../