Tehran: Afrika ni bara lenye fursa nyingi kwa makampuni ya Iran
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia Uratibu wa Diplomasia ya Uchumi amesema Afrika ni bara lenye fursa nyingi kwa makampuni ya Iran.
Mehdi Safari amesema hayo katika Kongamano la Uchumi la Iran na Afrika na kueleza kuwa, mkutano huo uliofanyika hapa Tehran umeangazia fursa, changamoto na suluhu za kustawisha uhusiano wa kiuchumi wa Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Afrika.
Shirika la habari la Mehr limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, miongoni mwa washiriki wa mkutano huo ni wakurugenzi na wawakilishi wa sekta binafsi na za umma, wekiwemo mameneja wa makampuni muhimu za Afrika.
Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia Uratibu wa Diplomasia ya Uchumi amesisitiza kuwa, nchi za bara Afrika zina soko kubwa na lenye fursa nyingi kwa makampuni ya Jamhuri ya Kiislamu.
Safari amebainisha kuwa, katika fremu ya sheria za kimataifa, daima kuna fursa mbali mbali kwa Iran na nchi za Afrika za kupanua mahusiano yao.

Afisa huyo ambaye pia ni Mkuu wa Kamisheni ya Pamoja ya Ustawi wa Biashara ya Iran na Afrika amesisitizia haja ya kuundwa ramani ya njia ya kupiga jeki mabadilishano ya kibiashara baina ya Iran na Afrika.
Kadhalika amesema kuna umuhimu wa kuendelezwa mikutano baina ya maafisa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Kamisheni ya Pamoja ya Ustawi wa Biashara ya Iran na Afrika, ili kufanikisha utekelezaji wa sera na makubaliano ya kibiashara baina ya Jamhuri ya Kiislamu na nchi za Kiafrika.