Kwesi Pratt: Iran ina mfumo madhubuti wa demokrasia
Mwandishi mashuhuri wa habari wa Ghana amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina mfumo madhubuti wa demokrasia.
Kwesi Pratt, mwandishi wa habari mwandamizi wa Ghana, ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na mwandishi wa habari wa IranPress huko Accra, mji mkuu wa Ghana, akizungumzia umuhimu wa uchaguzi na demokrasia nchini Iran. Amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeunda na kuendeleza mfumo imara wa kidemokrasia katika kipindi cha miaka 45 iliyopita na mfumo huo unaendelea kuimarika.
Amesema kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeonesha kuwa njia ya maendeleo inaweza kuchaguliwa kwa uhuru na kujitawala kisiasa na kuongeza kuwa, himaya na uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa harakati za kimapinduzi umekuwa na ufanisi katika kupunguza mateso ya watu wanaodhulumiwa.
Kwesi Pratt amepongeza kusimama kidete kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kukabilana na sera za kibabe za nchi za Magharibi na kusema mwenendo huo wa Iran wa kukabiliana na madola ya kibeberu unapaswa kuigwa na nchi nyingine.
Ijumaa wiki hii wananchi wa Iran watashiriki katika duru ya 12 ya uchaguuzi wa Bunge na wa 6 wa Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ambazo ni chaguzi za 40 na 41 katika kipindi cha miaka 45 iliyopita.