Feb 29, 2024 07:13 UTC
  • Marekani yatumia $12m kuwalinda wahalifu waliohusika na mauaji ya Jenerali Soleimani

Ripoti zinasema Idara ya Huduna za Siri ya Marekani inaripotiwa kutumia zaidi ya dola milioni 12 ili kuwalinda washauri wawili wa usalama wa rais wa zamani wa nchi hiyo, Donald Trump kwa kuhofia "vitisho" dhidi ya maisha yao kutoka Iran kwa ajili ya kulipiza kisasi mauaji ya kamanda mkuu wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Luteni Jenerali Qassem Soleimani aliyeuawa kigaidi na ndege isiyo na rubani ya Marekani akiwa safarini nchini Iraq.

Ripoti iliyofichuliwa na mtandao wa televisheni wa CBS inasema, John Bolton na Robert O'Brien walikuwa wakipewa ulinzi kwa karibu mwaka mmoja baada ya kuacha kazi Ikulu ya White House.

CBS imesema gharama ya jumla ya ulinzi kwa watu hao wawili ilikuwa $12,280,324, kulingana na mfululizo wa ripoti za Idara ya Usalama wa Nchi (DHS).

Ripoti ya CBS inasema "Bolton na O'Brien walikuwa wakipewa ulinzi kutokana na vitisho tarajiwa" kutoka Iran.

Kulingana na hati za DHS, ulinzi huo unahusisha "mawakala maalumu waliojitolea, saa 24 kwa siku, kulinda nyumba na maofisa hao wa serikali ya Marekani, pamoja na safari zao za ndani na nje ya nchi."

CBS imeripoti kuwa, maafisa kama Bolton na O'Brien hawapasi kupewa kiwango hiki cha ulinzi mara tu wanapoondoka ofisini; hata hivyo waliendelea kupewa ulinzi wenye gharama kubwa hata baada ya kuondoka Ikulu ya Rais wa Marekani, White House.

Itakumbukwa pia kwamba, shirika la habari la Associated Press lilifichua memo ya bunge mnamo Machi 2022 kwamba Wizara ya Mambo ya Nje imekuwa ikitumia dola milioni 2 kwa mwezi kutoa usalama wa wakati wote kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Trump, Mike Pompeo na Brian Hook, mjumbe wa zamani wa Marekani katika masuala ya Iran.

Trump alikuwa rais wa Marekani alipoamuru shambulio la anga lililomuua kigaidi Jenerali Soleimani, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Quds cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC), Januari 3, 2020.

Jenerali Soleimani alikuwa safarini nchini Iraq kwa mwaliko wa waziri mkuu wa wakati huo wa nchi hiyo.

Jenerali Soleimani

Baada ya mauaji hayo, Iran ilishambulia kambi ya jeshi la Marekani ya Ain Al-Asad nchini Iraq kwa makombora kadhaa. Iran imeapa kwamba watu wote waliohusika na mauaji ya Jenerali Soleimani watalipa gharama yake.