Kan'ani: Jeraha la Gazah halitafutika katika kumbukumbu za watu huru
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, jeraha la Gazah halitafutika katika kumbukumbu za watu huru.
Nassir Kan'ani amesema pia kuwa, aibu ya kuunga mkono na kunyamazia kimya mauaji ya umati na mauaji ya halaiki haitafutika katika mapaji ya nyuso ya wanaotoa madai uwongo ya haki za binadamu.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameandika katika mtandao wa kijamii wa "X" kuwa: Zaidi ya raia 100 wa Palestina waliokuwa wakisubiri kupokea misaada ya kibinadamu katika Mtaa wa Al-Rashid katika mji wa Gaza waliuawa shahidi na zaidi ya watu 800 walijeruhiwa kutokana na mashambulizi ya kinyama ya utawala wa Kizayuni.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran amesema kuwa, jinai hizi za Wazayuni maghasibu katu haziwezi kusahaulika.
Wizara ya Afya ya Palestina jana ilitangaza kuwa, wanajeshi wa Israel wamewauwa shahidi watu wasiopungua 104 waliokuwa katika umati uliokuwa ukisubiri kupatiwa misaada ya kibinadamu huko kusini mwa Gaza.
Watu walioshuhudia wameeleza kuwa mamia ya Wapalestina walikuwa wakisubiri kugawiwa misaada ya kibinadamu karibu na eneo lq Dowar al Nablusi wakati walipofyatuliwa risasi na wanajeshi wa utawala wa Kizayuni.
Ofisi ya vyombo vya habari ya Palestina imeeleza kuwa utawala wa Kizayuni ulikusudia kutekeleza mauaji hayo ya kutisha dhidi ya Wapalestina. Ofisi hiyo imelithumu jeshi la Israel kwa kuwauwa raia hao wa Kipalestina kwa damu baridi kwa sababu utawala huo ghsibu ulikuwa na taarifa kuhusu uwepo katika eneo hilo wa raia hao wa Kipalestina kwa ajili ya kupatiwa chakula na misaada mingine ya kibinadamu.