Ushiriki wa Wairani katika uchaguzi, jibu kwa misimamo ya uingiliaji kati hasi ya Merekani
(last modified Sat, 02 Mar 2024 13:41:26 GMT )
Mar 02, 2024 13:41 UTC
  • Ushiriki wa Wairani katika uchaguzi, jibu kwa misimamo ya uingiliaji kati hasi ya Merekani

Kushiriki kwa wananchi wa Iran katika uchaguzi wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wamaomchagua Kiongozi Mkuu, kwa mara nyingine tena, kumezima njama za wapinzani wa Jamhuri ya Kiislamu wakiongozwa na Marekani, za kuwakatisha tamaa wananchi ili wasishiriki katika upigaji kura.

Uchaguzi wa duru ya 12 ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge) na Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulifanyika jana Ijumaa kote nchini. Uchaguzi huo ulioanza  asubuhi saa mbili kamili, ulimalizika saa sita usiku baada ya muda wake kurefushwa mara kadhaa kutokana na mahudhurio makubwa ya watu. 

Tangu siku kadhaa kabla ya uchaguzi huo, kama ilivyokuwa katika chaguzi zilizopita nchini Iran, maafisa wa serikali ya Marekani walidai katika taarifa zao kwamba wananchi hawatashiriki katika zoezi hilo kwa sababu eti ni uchaguzi wa kimaonyesho. Maafisa wa Marekani, akiwemo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje na mwakilishi wa nchi hiyo katika masuala ya Iran, walijaribu kuhoji mfumo wa uchaguzi wa Iran kwa kutoa kauli zinazoingilia kati mambo ya ndani ya Iran. Matthew Miller, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, alidai siku ya Alhamisi, siku moja kabla ya uchaguzi wa Iran, kwamba idadi kubwa ya Wairani, kama ilivyo Marekani, hawatarajii kwamba uchaguzi huu utakuwa huru na wa haki.

Matthew Miller

Bila ya kutaja udhaifu wa wazi wa mfumo wa uchaguzi wa Marekani na maoni ya wachambuzi wa ndani na nje ya nchi hiyo wanaokiri kuwa mfumo huo ni dhaifu, Miller alidai kuwa utawala wa kisiasa wa Iran una mfumo wa kiutendaji, uchaguzi na mahakama usio wa kidemokrasia na usio wa uwazi. 

Naibu Mwakilishi Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran, Abram Paley, pia amedai kuwa serikali ya Iran inataka kutumia chaguzi hizo kama maonyesho ya demokrasia na kwamba watu wa Iran wanajua kwamba uchaguzi huu, vyovyote yatakavyokuwa matokeo yake, hautakuwa na maslahi kwao, na kwamba Marekani pia inakubaliana na mtazamo huo. Abram Peley amesisitiza udharura wa kuendelewa juhudi za Washington za kuishinikiza serikali ya Iran na kudai kuwa: "tutaendelea kusimama pamoja na wananchi wa Iran katika kupigania mustakbali huru na wa kidemokrasia."

Abram Paley

Madai haya ya Naibu Mwakilishi Maalumu wa Marekani katika Masuala ya Iran yametolewa licha ya kwamba, katika miaka ya hivi karibuni wananchi wa Iran wamepata madhara makubwa zaidi kutokana na vikwazo vya kikatili vilivyowekwa na Marekani.

Sambamba na matamshi ya uingiliaji kati hasi ya viongozi wa serikali ya Marekani na juhudi zao za kuwakatisha tamaa watu ili wasishiriki katika chaguzi za Bunge na Baraza la Wataalamu, kulifanyika kampeni pana na kubwa sana dhidi ya Iran ya kuwataka wananchi wasusie chaguzi hizo. Kampeni hizo ziliongozwa na wapinzani wa nje ya nchi na baadhi ya vikundi vya watu wenye siasa kali vya ndani. Pamoja na hayo yote, ushiriki wa takriban watu milioni 25 wa Iran katika uchaguzi huo unaashiria kushindwa kwa njama za wapinzani. Kwa hakika, licha ya mashinikizo na malalamiko yote ya kiuchumi, wananchi wa Iran walifanikiwa kushiriki kwa shauku katika uchaguzi huo na kuzima njama za kuudhoofisha mfumo wa Kiislamu.

Ujumbe muhimu zaidi wa wananchi wa Iran katika uchaguzi huo ni kwamba, ijapokuwa kuna baadhi ya matatizo ya kiuchumi na kijamii, lakini wanananchi wako macho kikamilifu mbele ya njama za maadui na harakati zinazopiga vita Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Ali Khamenei

Kuhusiana na suala hilo, Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jana baada ya kupiga kura katika uchaguzi wa Bunge la Baraza la Wataalamu aliwaambia waandishi wa habari kwamba, "hivi sasa watu wengi duniani wameelekeza macho yao nchini Iran; Marafiki zetu na watu wanaolitakia mema taifa la Iran, na vilevile wapinzani; Kwa sababu hii, kushiriki kwa hamasa katika uchaguzi, kutawafurahisha marafiki na kuwavunja moyo na kuwakatisha tamaa wasiolitakia mema taifa la Iran."