Mar 03, 2024 12:01 UTC
  • Azma ya Iran ya kupanua uhusiano na bara la Afrika

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jana Jumamosi aliwasili Algeria akiongoza ujumbe wa kiuchumi na kisiasa kwa ajili ya kuimarisha ushirikiano na asasi na jumuiya za kikanda na kimataifa, na pia kupanua uhusiano na nchi za bara la Afrika.

Kabla ya kuondoka Tehran kuelekea Algeria, Rais Ebrahim Raisi alisema: "Bara la Afrika kwa ujumla na hasa nchi za Kiislamu za bara hilo zina nafasi maalumu katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ninatumai kuwa, safari hii inaweza kuwa na nafasi kubwa katika kuimarisha uhusiano kati ya Asia Magharibi na Afrika Kaskazini."

Sera ya serikali ya Awamu ya 13 ya Iran ni kupanua uhusiano wa kisiasa na kiuchumi na nchi za bara la Afrika hususan nchi za Kiislamu za bara hilo; kwa mantiki hiyo Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitembelea Afrika mwezi Julai mwaka jana kwa mwaliko rasmi wa marais wa Kenya, Uganda na Zimbabwe. Katika safari hiyo jumla ya hati 21 za ushirikiano zilitiwa saini.

Raisi akizungumza na mwenzake wa Msumbiji, Filipe Nyusi 

Kwa sera hii ya Serikali ya Awamu ya 13, mpango wa kustawisha mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta na kupanua zaidi uhusiano wa kibiashara na Afrika ulishika kasi zaidi, na katika miaka miwili iliyopita, zaidi ya jumbe hamsini rasmi kutoka Afrika zilisafiri Iran na kutia saini mikataba mbalimbali. Pamoja na hayo, kiwango cha biashara kati ya Iran na nchi za Afrika bado kiko mbali na lengo la dola bilioni 10 kwa mwaka. Hivi sasa, uagizaji wa bidhaa wa barani Afrika kutoka nje unaripotiwa kuwa karibu dola bilioni 600, lakini sehemu ya Iran ya kiasi hicho haifikii dola bilioni 2. Hii ni licha ya kwamba, kuna nyuga nyingi za ushirikiano na uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na Afrika hususan katika nyanja za nishati, uhandisi na ufundi, uchukuzi, kilimo na madini. Kwa mfano tu, Afrika ina uwezo mwingi wa kuagiza bidhaa za Iran kama vile vifaa vya nyumbani, mazulia, vifaa vya umeme, zana za kusambaza na kugawa umeme, nguo na mashine za kilimo.

Suala la uchukuzi, dhamana na pia masuala ya kibenki na uhawilishaji fedha ni miongoni mwa matatizo yanayokwamisha upanuzi wa uhusiano wa kibiashara kati ya Iran na nchi za Afrika. Sayyid Ruhollah Latifi, Makamu Mkuu wa Iran and Africa Merchants Club, anasema kuhusu suala hili kwamba: Sehemu yetu ya biashara na bara la Afrika ni ndogo, na ili kuongeza kiwango cha biashara baina ya pande mbili kuna ulazima wa kutangaza bidhaa za Iran kwenye soko la Afrika, na kutoa ujuzi sahihi wa sheria na kanuni za masoko ya pande mbili, kuondoa vikwazo vya usafirishaji bidhaa na kuhawilisha fedha.

Rais wa Iran akiwa pamoja na Rais William Ruto wa Kenya

Mbali na nyanja za kiuchumi na kibiashara, upande wa kisiasa wa uhusiano na nchi za bara la Afrika pia ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nchi za Kiafrika zinaunda thuluthi moja ya nchi duniani; hivyo kupanua uhusiano na nchi hizo kunaweza kuisaidia Iran, ambayo iko chini ya vikwazo haramu vya nchi za Magharibi hususan Marekani, kupata uungaji mkono wa kimataifa. 

Ikumbukwe pia kwamba kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara la Afrika na karibu 50% ya wakazi wake ni Waislamu. Vilevile, nchi 50 kati ya 54 za bara hilo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), na harakati hii hadi sasa imetetea kwa kauli moja haki ya Iran ya kutumia sayansi na teknolojia ya nyuklia kwa njia ya amani.

Tags