Apr 20, 2024 08:17 UTC
  • Tehran: Vyombo vya habari vya Magharibi vinajaribu kugeuza kushindwa Israel kuwa ushindi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian amesema kuwa quadcopter tatu za kigeni (videge vigogo visivyo na rubani) zilizotunguliwa na walinzi wa anga wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mji wa kati wa Isfahan hazikusababisha uharibifu wala majeruhi yoyote ndani ya nchi.

Amir-Abdollahian amesema hayo katika mkutano wake na mabalozi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kuongeza kuwa: "Katika jaribio la kukata tamaa, vyombo vya habari vinavyouunga mkono utawala wa Kizayuni Israel vinajaribu kuutengenezea ushindi bandia utawala huo kutokana na kushindwa kwao mara kwa mara." 

Sauti za mlipuko zilisikika usiku wa kuamkia Ijumaa ya jana karibu na Isfahan na mji wa kaskazini-magharibi wa Tabriz baada ya mifumo ya ulinzi wa anga ya Iran kutungua "vyombo vidogo vilivyotiliwa shaka."

Jeshi la Iran limetungua quadcopter tatu za kigeni

Maafisa wa Iran wamesema vituo muhimu katika mkoa wa Isfahan hususan vituo vya nyuklia viko salama kabisa na hakuna matukio yoyote yaliyoripotiwa.

Wakati huo huo, katika matamshi yake, Amir-Abdollahian amesema mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Israel hapo tarehe 13 Aprili yaliyopewa jina la Operesheni True Promise - yalifanyika katika fremu ya haki halali ya kujilinda na kwa mujibu wa sheria za kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza kuwa: "Ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu ilikuwa na uwezo kutekeleza operesheni hiyo kwa kiwango kikubwa zaidi, lakini ililenga tu vituo vya kijeshi vya utawala wa Kizayuni ambavyo vilitumiwa kushambulia balozi wa nchi yetu huko Damascus." 

Amesema kuwa, Iran ilifanikiwa kutimiza malengo yake "ndani ya mfumo wa jibu la chini kabisa" na kufikisha ujumbe wake kwa Israel.