Apr 23, 2024 08:36 UTC
  • Raisi: Iran itaendelea kuunga mkono uhuru wa Syria

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amesema Jamhuri ya Kiislamu itasimama kidete pamoja na Syria na itaendelea kuunga mkono uhuru wake na umoja wa ardhi yake.

Katika ujumbe kwa Rais wa Syria Bashar al-Assad siku ya Jumatatu, Raisi amempongeza yeye na watu wa Syria kwa mnasaba wa siku ya kitaifa ya nchi hiyo ya Kiarabu.

Amesema Iran kwa mara nyingine tena inasisitiza umuhimu wa kuwafukuza wavamizi kutoka Syria. Rais wa Iran ameeleza imani yake kuwa Tehran na Damascus zitaweza kuchukua hatua muhimu kuelekea kustawisha uhusiano mpana kwa kutumia uwezo wao mkubwa.

Amesisitiza kuwa pande hizo mbili zinaweza pia kukuza ushirikiano wa kikanda kwa madhumuni ya kupanua amani, utulivu na maendeleo katika eneo hilo katika nyanja zote.

Marekani ilivamia kijeshi Syria mwaka 2014 kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi la Daesh. Vikosi vya Marekani vinaendelea kubakia katika ardhi ya Syria kinyume cha sheria pamoja na kuwa serikali ya Syria na washirika wake walilitimua kundi la kigaidi kutoka maeneo yote ya Syria mwishoni mwa 2019. Syria inasisitiza kuwa majeshi ya Marekani yanaendelea kubakia nchini humo kinyume cha sheria kwa lengo la kupora utajiri wa nchi hiyo haa mafuta ya petroli na kuung mkono magaidi wa Daesh waliosalia nchini humo.