May 23, 2024 12:32 UTC
  • Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran azikwa mjini Rey, mkoani Tehran

Mwili wa Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliyekufa shahidi katika ajali ya helikopta iliyotokea Jumapili iliyopita kaskazini magharibi mwa nchi umezikwa leo katika Haram ya Shah Abdol-Azim katika mji wa Shahre-Rey, kusini mwa Tehran.

Maelfu ya wananchi wa Waislamu wa Iran wamejitokeza kuuaga na kuuzika mwili wa mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Jamhuri ya Kiislamu. Kadhalika maafisa wa ngazi za juu wa Iran wamehudhuria maziko hayo mjini Rey.

Miongoni mwa shakhsia walioshiriki kwenye maziko ya Amir-Abdollahian ni aliyekuwa Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran, Mohammad Javad Zarif, Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (IRIB), Peyman Jebeli, Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran (AEOI), Dakta Ali Larijani, aliyekuwa Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), na Sayyid Abbas Araqchi, Katibu wa Baraza la Kistratajia la Mahusiano ya Kigeni la Iran.

Viongozi wengine wa ngazi za juu walioshiriki katika shughuli ya kuuaga mwili wa Amir-Abdollahian ni Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Baqer Qalibaf na Nasser Kan'ani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, miongoni mwa mwengine.

Dakta Zarif akimfariji Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Shahidi Amir-Abdollahian daima amekuwa akitilia mkazo kusitishwa mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kuwaunga mkono wananchi madhulumu wa Palestina.

Aidha atakumbukwa kwa kufanya kazi kubwa ya kufufua na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia, kibiashara, kiuchumi na kiutamaduni wa Iran na nchi mbalimbali duniani hasa za Afrika na mataifa ya Kiislamu na Kiarabu ya Asia Magharibi na Ghuba ya Uajemi.

Tags