May 04, 2024 06:56 UTC
  • Abdollahian aelekea Gambia kushiriki mkutano wa OIC, unajadili changamoto za Waislamu hususan Palestina

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameondoka Tehran kuelekea Banjul, mji mkuu wa Gambia kwa ajili ya kushiriki katika mkutano wa 15 wa Wakuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, OIC.

Katika mkutano huo, Hossein Amir Abdollahian,  ataeleza misimamo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu matukio mbalimbali ya Ulimwengu wa Kiislamu, kieneo na kimataifa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia atakutana na kujadiliana na baadhi ya maafisa wa nchi za Kiislamu pembezoni mwa mkutano huu.

Mkutano huo wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu unaoanza leo Jumamosi na kuendelea hadi kesho Jumapili, kwa kaulimbiu kuu ya "kukuza umoja na mshikamano kwa njia ya mazungumzo juu ya maendeleo endelevu", unajadili masuala na changamoto mbalimbali za Ulimwengu wa Kiislamu, hasa suala la Palestina na hali ya sasa ya Ukanda wa Gaza.

Gambia ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano wa 15 wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu, inapatikana katika eneo la Magharibi mwa Afrika.

Gambia itachukua uenyekiti wa mkutano huo kutoka Saudi Arabia na itakuwa mwenyekiti wa OIC kwa kipindi cha miaka mitatu ijayo.

Tags