May 25, 2024 07:30 UTC
  • Khitma ya shahidi Raisi na wenzake katika kikao cha wajumbe wa OIC

Ofisi ya Umoja wa Mataifa mjini Geneva imeandaa kikao cha Khitma kwa ajili ya marehemu Rais wa Iran Ebrahim Raisi na Waziri wa Mambo ya Nje Hossein Amir-Abdollahian, waliokufa shahidi katika ajali ya helikopta kaskazini magharibi mwa Iran siku ya Jumapili.

Kikao hicho kiliendeshwa na wajumbe wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), waliomuenzi marehemu rais wa Iran na wenzake.

Ali Bahraini, balozi wa Iran katika mashirika ya Umoja wa Mataifa yenye makao yake makuu mjini Geneva, alitoa hotuba katika hafla hiyo, akiangazia namna hayati Raisi alivyotetea maadili ya Kiislamu katika uga wa kimataifa.

Ameongeza kuwa: "Jumuiya ya Kiislamu haitasahau utetezi mkali wa Raisi wa Qur'ani Tukufu dhidi ya vitendo viovu vya baadhi ya wahalifu wanaoungwa mkono na nchi za Magharibi. Katika kikao cha 78 cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, aliinua Al-Mus'haf Al-Sharif juu ya kichwa chake huku akitoa hotuba ya kutetea kitabu hicho kitakatifu."

Mashahidi Raisi na Amir Abdollahian

Bahraini pia aliashiria juhudi za Raisi za kukuza umoja kati ya Waislamu duniani kote. "Katika kutekeleza sera kuu za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, hayati rais wa Iran na Waziri wa Mambo ya Nje walijitahidi kuimarisha umoja wa ulimwengu wa Kiislamu."

Hali kadhalika balozi huyo amesema: "Yeye (Amir-Abdollahian) alifanya kazi kwa azma kubwa ya kuimarisha uhusiano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mataifa ya Kiislamu, kwa kufuata sera kuu za Iran, na kuchukua hatua muhimu katika suala hili."

Balozi huyo aidha ameashiria juhudi kubwa za Waziri wa Mambo ya Nje Amir-Abdollahian za kurejesha haki za wananchi wa Palestina na kuikomboa Quds tukufu akimtaja kuwa ni miongoni mwa Mujahidina waliofanya kampeni katika harakati za kuikomboa Palestina. Ameendelea kusema kuwa: "Tunatumai kwamba urithi wao wa haki, amani, na ustawi utaendelea kufaidi taifa la Iran, jumuiya ya Kiislamu na ubinadamu."

Mjumbe huyo wa Iran amesisitiza kuwa, Iran itaendelea kwa dhati katika "njia iliyobarikiwa ya kuimarisha umoja wa Kiislamu na kustawisha ujirani mwema."