Jun 26, 2024 02:19 UTC
  • HRW yataka kutumwa ujumbe wa UN nchini Sudan ili kuwalinda raia

Shirika la kutetea haki za binadamu la Human Rights Watch limetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kufanya kazi na Umoja wa Afrika haraka iwezekanavyo ili kutuma ujumbe wa kulinda raia nchini Sudan.

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa X, shirika hilo la kutetea haki za binadamu limesema kwamba, pande zinazopigana "zimeua mamia ya raia na kulazimisha makumi ya maelfu ya wengine kuwa wakimbizi."

Human Rights Watch imeashiria mauaji ya mamia ya raia katika mji wa El Fasher katika jimbo la Darfur Kaskazini, magharibi mwa Sudan, na kukimbia makazi makumi ya maelfu ya wengine.

Wakimbizi nchini Sudan

Mapema Jumatatu, Umoja wa Mataifa ulitangaza kuwa takriban watu 143,000 wamekimbia makazi yao kutoka El Fasher, kutokana na mapigano yanayoendelea kati ya jeshi la Sudan na Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF).

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Masuala ya Kibinadamu ilisema katika taarifa yake kwamba, "Sudan inaendelea kutumbukia katika machafuko, huku kukiwa na hali mbaya zaidi ya binadamu na athari za kutisha za mzozo huo kwa raia huko El Fasher na maeneo mengine yenye mizozo."

Tangu katikati ya Aprili 2023, jeshi la Sudan, likiongozwa na Abdel Fattah al-Burhan, na Vikosi vya Msaada wa Haraka vinavyoongozwa na Mohamed Hamdan Dagalo, vimekuwa vikipigana vita vilivyosababisha vifo vya watu zaidi ya 15,000; na kulingana na takwimu za Umoja wa Mataifa, takriban Wasudani milioni 8.5 wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na vita hivyo.