May 26, 2024 07:23 UTC
  • Ejei: Sera za ndani na nje za Iran zitaendelea kuwa na nguvu zaidi kuliko hapo awali

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema katika mazungumzo na Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq kuwa; Sera za ndani na nje za Iran zitaendelea kuimarika zaidi kuliko hapo awali.

Hujjatul Islam wal Muslimin Gholamhossein Mohseni-Ejei jana alikuwa na mazungumzo na Faiq Zidan Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq ambaye amefika mjini Tehran akiambata na viongozi wengine wa ngazi ya juu wa nchi hiyo. Huku akitoa shukrani zake kwa serikali na wananchi wa Iraq kwa mkono wao wa pole na salamu za rambirambi kufuatia kufa shahidi katika ajali ya helikopta Rais Sayyid Ebrahim Rais wa Iran na maafisa wengine aliokuwa nao, Ejei amesema: 'Taifa la Iran limepoteza shakhsia dhimu katika ajali ya karibuni lakini pamoja na hayo wamesalimu amri mbele ya irada na mapenzi ya Mwenyezi Mungu.'

Ejei ameongeza kuwa: Kama ilivyobainishwa katika miongozo ya Kiongozi Muadhamu, sera za ndani na nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zitaendelea kuwa na nguvu na kuimarika zaidi; na ni wazi kuwa hakuna jambo lolote lililokwamisha na litakalokiwamisha uendeshaji wa nchi baada ya kufa shahidi Rais Raisi, bali watumishi na wananchi wa Iran huku wakiwa wameshikamana wanaendelea kuchapa kazi kwa kuhisi pakubwa kuwa na majukumu na maasulia; na inshaAllah katika chini ya siku 50 wananchi wa Iran watashiriki katika uchaguzi na kumchagua  Rais mpya wa nchi hii. 

Mohsein Ejei

Katika mazungumzo hayo, Faiq Zidan Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama la Iraq pia ameeleza kuwa anaona kuna ulazima wa kuwasilisha salamu za rambirambi na mkono wa pole kwa niaba ya majaji wa Iraq kufuatia kufa shahidi Rais wa Iran. Amesema, katika kipindi cha uongozi wa  Sayyid Ebrahim Raisi akiwa Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran na baada ya hapo, nchi mbili za Iran na Iraq ziliweza kushirikiana katika kubuni misingi ya uendeshaji wa kesi muhimu.  

Tags