Iran yataka jamii ya kimataifa kuishinikiza Israel kuheshimu maamuzi ya ICJ
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i112806-iran_yataka_jamii_ya_kimataifa_kuishinikiza_israel_kuheshimu_maamuzi_ya_icj
Iran imeutaka Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili utii amri zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vya utawala huo kwenye Ukanda wa Gaza.
(last modified 2024-06-11T08:40:10+00:00 )
Jun 11, 2024 08:40 UTC
  • Iran yataka jamii ya kimataifa kuishinikiza Israel kuheshimu maamuzi ya ICJ

Iran imeutaka Umoja wa Mataifa kuushinikiza utawala wa Kizayuni wa Israel ili utii amri zilizotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) dhidi ya vita vya mauaji ya kimbari vya utawala huo kwenye Ukanda wa Gaza.

Katika barua iliyotumwa kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres siku ya Jumatatu, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa muda wa Iran Ali Bagheri Kani alisema Umoja wa Mataifa una wajibu wa kuzitaka nchi zote wanachama kuacha kushirikiana na utawala vamizi wa Israel kwani kushirikiana na utawala huo kunamaanisha kuwa mshirika wa jinai zake.

Katika kesi iliyoletwa na Afrika Kusini dhidi ya Israel, ICJ, mahakama kuu ya Umoja wa Mataifa, ilitoa hatua tatu za muda Januari 26, Machi 28 na Mei 24.

ICJ iliiamuru Israel kuchukua hatua zote ndani ya uwezo wake kuzuia mauaji ya kimbari huko Gaza, kuruhusu upatikanaji wa chakula bila vikwazo katika eneo la Palestina lililozingirwa, na kusitisha mara moja uvamizi wake wa kijeshi katika mji wa kusini wa Rafah. Israel imepuuza maagizo hayo yote ya ICJ.

Mauaji ya kimbari Gaza

Kadhalika katika barua yake hiyo Ali Bagheri Kani amesema jumuiya ya kimataifa inapaswa kukomesha haraka ukatili unaoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni katika ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na kuwalinda raia wasio na hatia.

Chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa, Bagheri Kani alisema, mataifa yote, haswa yale yanayotoa msaada kwa Israel, yana wajibu wa kisheria wa kuzuia mauaji ya halaiki kwa kusitisha misaada kwa utawala huo wa kimbari.

Israel ilianzisha mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya harakati ya Hamas Palestina kutekeleza operesheni yake ya kihistoria dhidi ya utawala huo ghasibu ili kulipiza kisasi dhulma zinazozidi kufanywa na utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.

Hadi sasa utawala wa Tel Aviv umeshaua Wapalestina wasiopungua 37,124 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 84,712 katika Ukanda wa Gaza.