Wagombea urais wa Iran wawasilisha mipango huku kampeni za televisheni zikianza
Wagombea urais nchini Iran wameanza kubainisha mipango yao kuhusu ustawi wa nchi huku kampeni za uchaguzi zikianza kushika kasi.
Mgombea urais Mohammad Baqer Qalibaf amesisitiza haja ya "mabadiliko" katika sekta zote za nchi kwa njia ya "usimamizi wa kidijitali."
Akizungumza katika muda sawa uliotengewa wagombea wote kwenye televisheni ya kitaifa, Qalibaf aliashiria kuhusu maswala ya kiuchumi ambao msingi wake ni uwazi.
Aidha katika matamshi yake, Qalibaf, ambaye kwa sasa ni spika wa bunge, alisema kuwa amechagua kauli mbiu ya "huduma na maendeleo" kwa ajili ya kampeni yake ya uchaguzi.
Siku ya Jumatatu pia, mgombea mwingine Masoud Pezeshkian alisema anafuata sera ya "uthabiti," akibainisha kwamba mabadiliko ya mwelekeo yatazuia nchi kufikia ukuaji unaotarajiwa na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei.
Alipoulizwa kuhusu Mpango wa Saba wa Maendeleo ya Taifa, alijibu, “Hatutaandika mpango mpya na hatutatangaza sera mpya nchini.
Aidha ameonya kuwa kukosekana utulivu na uthabiti kutawafanya wawekezaji wa ndani kuwa na shaka iwapo watawekeza nchini na hivyo kuwasukuma kuondoka Iran.
Mgombea mwingine wa urais Amir Hossein Qazizadeh Hashemi alisema Jumatatu kwamba sekta za uchumi zinazosimamiwa na serikali zinapaswa kukabidhiwa sekta binafsi kupitia mchakato wa ubinafsishaji wa kweli.
Alibainisha kuwa kauli mbiu ya kampeni yake ni "serikali ya watu na serikali ya familia." Qazizadeh Hashemi, ambaye ni mkuu wa Wakfu wa Mashahidi na Masuala ya Maveterani, alisema kuwa amejitolea kufuata njia ya hayati Rais Ebrahim Raisi, ikiwa ni pamoja na kutetea haki, fursa sawa na mapambano dhidi ya rushwa.
Wagombea sita wameidhinishwa kuwania urais katika uchaguzi wa Juni 28. Kura hiyo iliitishwa baada ya Rais Raisi kufa shahidi akiwa na watu wengine saba mnamo Mei 19, wakati helikopta iliyokuwa imewabeba ilipoanguka katika eneo la milima kaskazini-magharibi mwa Iran huku kukiwa na hali ya ukungu.