Matarajio ya kimkakati ya Kiongozi Muadhamu kwa Vyombo vya Mahakama nchini
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i113262-matarajio_ya_kimkakati_ya_kiongozi_muadhamu_kwa_vyombo_vya_mahakama_nchini
Akizungumza jana Jumamosi katika hadhara ya viongozi wa Vyombo vya Mahakama nchini, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza matarajio yake kutoka kwa muhimili huo wa dola.
(last modified 2024-06-23T08:05:43+00:00 )
Jun 23, 2024 08:05 UTC
  • Matarajio ya kimkakati ya Kiongozi Muadhamu kwa Vyombo vya Mahakama nchini

Akizungumza jana Jumamosi katika hadhara ya viongozi wa Vyombo vya Mahakama nchini, Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza matarajio yake kutoka kwa muhimili huo wa dola.

Tarehe 28 Juni mwaka 1981 ni tarehe aliyouawa shahidi na magaidi wa Munafiqin, Ayatollah Sayyid Muḥammad Beheshtī, Mkuu wa pili wa Vyombo vya Mahakama vya Iran, akiwa na wenzake wengine 72. Kwa sababu hiyo, tarehe 21 hadi 27 Juni kila mwaka imetengwa hapa nchini kama Wiki ya Mahakama kwa ajili ya kuenziwa chombo hicho muhimu cha mahakama na pia kumkumbuka Ayatollah Sayyid Muḥammad Beheshti na wenzake wengine waliouawa shahidi katika tukio hilo la kigaidi.

Shahidi Ayatollah Sayyid Muḥammad Beheshtī

Kwa mnasaba huo wa Wiki ya Mahakama nchini, Gholamhossein Mohseni Ajeei, Mkuu wa Vyombo vya Mahakama na viongozi wengine wa tawi hilo la dola walikutana Jumamosi na Ayatullah Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ili kusikia maoni na mitazamo yake kuhusu utendaji wa chombo hicho.

Katika kikao hicho, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alizungumzia baadhi ya nukta muhimu ambazo ni miongoni mwa matarajio yake kutoka kwa mfumo wa mahakama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ayatullah Khamenei akizungumza na wakuu wa Vyombo vya Mahakama nchini

Matarajio ya kwanza ya Kiongozi Muadhamu ni kwamba majaji wazingatie uadilifu katika hali zote za kazi zao. Uadilifu ndio moyo na nguzo ya shughuli za mahakama. Matarajio muhimu zaidi ya wananchi pia kwa mhimili wa mahakama ni kuzingatiwa haki na uadilifu katika utolewaji maamuzi ya mahakama bila kuzingatia nafasi na vyeo vya watu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu pia alisisitiza nukta hii katika kikao chake cha jana na viongozi wa Vyombo vya Mahakama ambapo alisema kuwa vyombo hivyo vinapasa kufanya kazi kwa namna ambayo itawafanya wananchi kiitazama mahakama kama kimbilio na kitovu cha kutekelezwa haki bila upendeleo.

Ujasiri wa majaji katika kutoa maamuzi ya kiadilifu ni matarajio mengine ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.

Kwa maneno ya Kiongozi Muadhamu, ujasiri ni jambo linaloimarisha uadilifu wa mahakama na kuzuia upendeleo usio wa haki kwa marafiki na kutolewa hukumu zisizo za kiadilifu kwa maadui na wapinzani.

Hali kadhalika ujasiri unaweza kuimarisha uhuru wa mfumo wa mahakama, jambo ambalo daima limekuwa likisisitizwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Jukumu la mahakama ni kutekeleza uadilifu kwa ujasiri na bila kuyumba. 

Kupunguzwa muda wa kushughulikiwa kesi na kasi katika suala hilo ni miongoni mwa matarajio mengine ya Kiongozi wa Mapinduzi, kwa sababu kasi inayoandamana na haki na ujasiri katika uwanja huo itaongeza ridhaa ya wananchi kwa mfumo wa mahakama na kupunguza upotezaji wakati katika kushughulikiwa kesi za watu.

Wakati huo huo, matokeo muhimu ya kuzingatia viashiria hivi kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu ni kupewa umuhimu "afya ya akili na kisaikolojia ya watu."

Matarajio mengine muhimu aliyonayo Ayatullah Ali Khamenei kwa mfumo wa mahakama ni kwamba maamuzi yatolewe kwa mujibu wa kanuni na sheria za Kiislamu.

Kwa miongo kadhaa sasa, ulimwengu wa Magharibi umekuwa ukijaribu kutambulisha thamani na maadili ya Magharibi kama maadili bora zaidi kwa ajili ya wanadamu na hivyo kuzishinikiza nchi zingine zitekeleze maadili hayo katika mahakama zao za ndani.

Hayo ni pamoja na ukweli kwamba dini ya Kiislamu kwa miongo mingi imekuwa mwanzilishi na mtekelezaji muhimu wa sheria na maadili ya haki za binadamu.

Kuhusiana na suala hilo, katika kikao chake cha jana na viongozi na maafisa wa Vyombo vya Mahakama,  Kiongozi Muadhamu  alisisitiza kuwa, majaji hawapaswi kuegemea misingi ya haki za binadamu ya Magharibi katika kutoa hukumu zao mahakamani.