Jul 02, 2024 11:57 UTC
  • Kan'ani: Kukaa kimya mkabala wa jinai za Wazayuni ni mbali na ubinadamu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuwa kunyamaza kimya jamii ya kimataifa mkabala wa jinai za Wazayuni huko Ukanda wa Gaza ni mbali na utu na ubinadamu.

Nasser Kan'ani Chafi ameashiria jinai zisizokwisha za kila uchao za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza na kuandika katika mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Kukaa kimya na kuwepo mitazamo tofauti mkabala wa jinai zote hizo na za kutisha zinazotekelezwa na Israel katika Ukanda wa Gaza ni mbali na uwajibikaji wa kibiandamu na kimaadili; na zinapingwa na kulaaniwa katika mahakama ya dhamiri ya binadamu na katika mahakama ya Mwenyezi Mungu."  

Jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza 

Kan'ani Chafi amesema maumivu na masaibu yaliyosababishwa kwa miili ya Wapalestina na wakazi wa Ukanda wa Gaza hayaelezeki na kuongeza: "Wajibu wa Marekani na waungaji mkono wengine wa utawala unaotenda jinai wa Israel katika kuendelea jinai za kutisha huko Ukanda wa Gaza si mdogo kuliko wa utawala huo."

Siku 270 zimepita sasa tangu kuanza vita dhidi ya Gaza huku utawala wa Kizayuni ukiendeleza mashambulizi yake katika eneo hilo. Ndege za kivita za utawala wa Kizayuni leo asubuhi zimeshambulia miji ya Rafah na Khan Younis, kusini mwa Ukanda wa Gaza. 

Wizara ya Afya ya Palestina pia imetangaza katika takwimu zake mpya kuwa Wapalestina 37,900 wameuliwa shahidi na 87,060 kujeruhiwa tangu Israel ianzishe vita dhidi ya Gaza Oktoba mwaka jana. 

Tags