Iran katika maombolezo ya Tasua, yaitaka dunia ikabiliane na jinai za Israel
(last modified Mon, 15 Jul 2024 13:25:36 GMT )
Jul 15, 2024 13:25 UTC
  • Iran katika maombolezo ya Tasua, yaitaka dunia ikabiliane na jinai za Israel

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran sanjari na kutoa mkono wa pole kwa Waislamu kote duniani ambao hii leo wapo katika maombelezo ya kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS, ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua za kivitendo za kusimamisha jinai na mauaji ya kimbari yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Nasser Kan'ani amesema hayo leo Jumatatu katika ujumbe alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X na kuongeza kuwa: Natoa mkono wa pole kwa Waislamu, Mashia na wapenda haki kote duniani wanaofungamana na chuo cha Imam Hussein AS, kwa mnasaba wa maombolezo ya Tasua ya Imam huyo wa 3 wa Mashia, na mashahidi wengine wa mapambano ya Karbala ya mwaka 61 Hijria.

Amewataka Waislamu kote duniani kuiga mfano wa Imam Hussein AS wa kusimama kidete dhidi ya dhulma na ukandamizaji, na kufanya hima kukabiliana na jinai za kinyama za Wazayuni na waungaji mkono wao dhidi ya Wapalestina wa Gaza.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Nasser Kan'ani amesisitiza kuwa: Sisi ni taifa la Imam Hussein AS.   

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran

Huku akiashiria jinai mpya iliyofanywa na utawala wa Kizayuni katika eneo la Al-Mawasi huko Khan Yunis, kusini mwa Ukanda wa Gaza, Kan'ani amekosoa vikali kimya cha jamii ya kimataifa mkabala wa mauaji dhidi ya wakimbizi wa Palestina wasio na ulinzi wala hatia katika eneo hilo ambalo utawala wa Kizayuni ulidai ni salama kwa ajili ya kukimbilia Wapalestina. 

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amebainisha kuwa, utawala katili wa Israel unaendelea kumwaga damu za Wapalestina kutokana na undumakuwili wa baadhi ya madola duniani, na ungaji mkono wa hali na mali wa Marekani na nchi za Ulaya.