Bagheri Kani na Rais wa Baraza Kuu la UN wajadili mauaji ya Gaza
(last modified Tue, 16 Jul 2024 07:44:45 GMT )
Jul 16, 2024 07:44 UTC
  • Bagheri Kani na Rais wa Baraza Kuu la UN wajadili mauaji ya Gaza

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuna udharura wa kuchukuliwa hatua za kivitendo ili kukomesha jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Ali Bagheri Kani alitoa mwito huo jana Jumatatu katika mkutano wake na Dennis Francis, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA) huko New York, ambapo walijadili matukio ya hivi sasa ya Ukanda wa Gaza.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran yuko New York kushiriki vikao viwili vya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amelipongeza Baraza Kuu la UN kwa kuchukua hatua za kujaribu kukomesha mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, ikiwemo kupasisha maazimio kadhaa.

Hii ni katika hali ambayo, idadi ya mashahidi wa Kipalestina waliouawa tangu kuanza hujuma za kinyama za jeshi la utawala wa Kizayuni huko Gaza (Oktoba 7, 2023) imekaribia watu 39,000.

Bagheri Kani (kushoto) na Rais wa Baraza Kuu la UN mjini New York

Kwa upande wake, Dennis Francis, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ameishukuru Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa juhudi zake za kuimarisha usalama na uthabiti katika eneo la Asia Magharibi kwa kuwa na mahusiano mazuri na majirani zake.

Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye leo Jumanne na kesho anatazamiwa kushiriki mkutano wa Baraza la Usalama utakaojadili misimamo na siasa za pande kadhaa, amesema Jamhuri ya Kiislamu itatumia jukwaa hilo kuendelea kupigania haki za msingi za Wapalestina, na kubainishia dunia jinai za Wazayuni.