Iran yasema Marekani haitekelezi ipasavyo JCPOA
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i11449-iran_yasema_marekani_haitekelezi_ipasavyo_jcpoa
Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameikosoa Marekani kwa kushindwa kutekeleza ipasavyo makubaliano ya nyuklia ya Vienna, mwaka mmoja tangu yatiwe saini nchini Austria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2016 23:51 UTC
  • Iran yasema Marekani haitekelezi ipasavyo JCPOA

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameikosoa Marekani kwa kushindwa kutekeleza ipasavyo makubaliano ya nyuklia ya Vienna, mwaka mmoja tangu yatiwe saini nchini Austria.

Akiongea jana Jumapili kwa mnasaba wa kutimia mwaka mmoja tangu kutiwa saini makubaliano hayo, Ali Akbar Velayati amesema, Marekani imekataa kuondoa vikwazo vya kidhalimu dhidi ya Iran na hilo ni ithibati tosha kuwa haitekelezi makubaliano hayo.

Hata hivyo Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa amekariri kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itaendelea kutekeleza wajibu wake katika makubaliano hayo yaliyopewa jina la Utekelezaji wa Mpango wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA). Amezipa changamoto nchi za Ulaya kuheshimu kikamilifu na kwa vitendo makubaliano hayo yaliyoanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka huu. Haya yanajiri siku chache baada ya Rais Hassan Rouhani wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kusema kuwa Tehran itaendelea kuheshimu na kutekeleza makubaliano ya nyuklia ya Vienna, lakini alionya kuwa haitasita kutoa jibu iwapo upande wa pili utaacha kutekeleza makubaliano hayo ipasavyo.

Makubaliano hayo ya nyuklia yaliyofikiwa Julai 14 mwaka jana mjini Vienna Austria kati ya Iran na Kundi la 5+1, licha ya kuanza kutekelezwa mwezi Januari mwaka huu, lakini Tehran imekuwa ikilalamika namna upande wa pili wa makubaliano hayo unavyokwenda mwendo wa kinyonga katika utekelezaji wake.