Iran: Israel imetengwa zaidi kisiasa duniani baada ya kumuua kigaidi Haniyah
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, kulaaniwa Israel kote duniani kwa mauaji ya Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas), Ismail Haniyah kumezidisha kutengwa kisiasa kwa utawala huo wa Kizayuni.
Shirika la Habari la Iran (IRNA) limeripoti kuwa, Ali Baqeri Kani, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema hayo jana Alhamisi alipoonana na kufanya mazungumzo na Waleed Abdulkarim El Khereiji, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Saudi Arabia, pambizoni mwa kikao dha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) mjini Jeddah.
Amebainisha kuwa, utawala wa Israel ulikuwa na matumaini kuwa, kutengwa kwake kisiasa kungepungua kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya nchi za eneo, lakini utawala huo umetengwa hata zaidi kufuatia shutuma kali za waliwemngu kwa mauaji ya Haniyah mjini Tehran, ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Jana Alkhamisi pia, mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran katika mahojiano na shirika la habari la AFP mjini Jeddah alisema kuwa, Israel ilifanya makosa ya kistratijia kwa kumuua Kiongozi wa Hamas, Ismail Haniyah, jinai ambayo anasema itaudhuru utawala huo pandikizi na kuufanya ulipe gharama kubwa.
Bagheri Kani amesema kuwa, Israel ina nia ya kueneza mzozo wa Ukanda wa Gaza katika nchi nyingine za eneo na kusisitiza kuwa, utawala huo ghasibu hauna uwezo na ubavu wa kuingia vitani na Iran.
El Khereiji kwa upande wake ameishukuru Iran kwa kuomba kufanyika kwa mkutano wa OIC na kusema kuwa, nchi zote zilizoshiriki kikao hicho zinaunga mkono Tehran na kulaani utawala ghasibu wa Israel kwa uvamizi wake dhidi ya ardhi ya Iran.
Aidha ameutaja mkutano wa Jeddah kuwa mzuri na wenye mafanikio makubwa, akieleza kuwa ulifanyika ndani ya fremu ya juhudi za pamoja za nchi za Kiislamu kukabiliana na uchokozi wa utawala haramu wa Israel.