Iran: Usitishaji vita Ghaza hauna uhusiano wowote na haki yetu ya kujibu mapigo kwa ugaidi wa Israel
Aug 10, 2024 03:29 UTC
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imesema, haki ya Jamhuri ya Kiislamu ya kulipiza kisasi dhidi ya ugaidi wa Israel ndani ya Iran haina uhusiano wowote na mazungumzo ya kusitisha mapigano yanayoendelea katika Ukanda wa Ghaza.
Ofisi hiyo ilitoa tamko hilo jana Ijumaa ilipoulizwa kama Iran itaghairi kutoa jibu kwa utawala wa Kizayuni wa Israel hadi mazungumzo ya wiki ijayo kuhusu usitishaji vita huko Ghaza, ambayo imekuwa ikiandamwa na mashambulio ya kinyama na mauaji ya kimbari ya utawala huo haramu tangu Oktoba mwaka jana.
Taarifa ya ofisi hiyo imesema: "kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu huko Ghaza ni kipaumbele chetu. Makubaliano yoyote ambayo Hamas itayakubali yatakubaliwa na sisi".
Ofisi ya uwakilishi wa kudumu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imetamka bayana: "usalama wetu wa taifa na mamlaka yetu ya kujitawala vimekiukwa wakati wa kitendo cha hivi karibuni cha kigaidi cha utawala wa Israel. Tuna haki ya kujilinda kisheria na hili halina uhusiano wowote na usitishaji vita wa Ghaza".
Taarifa ya ofisi hiyo imeongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu inatumai kwamba jibu lake dhidi ya utawala Kizayuni litakamilika kwa wakati na kwa njia ambayo haitadhuru uwezekano wa kusitishwa mapigano.
Ismail Haniya, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS na mmoja wa walinzi wake waliuawa shahidi alfajiri ya kuamkia Jumatano ya tarehe 31 Julai hapa mjini Tehran. Kufuatia mauaji hayo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) lilitangaza kuwa Haniya aliuawa shahidi kwa "kombora la masafa mafupi" lililorushwa kutokea nje ya jengo la makazi aliyofikia.
Uongozi wa kisiasa na kijeshi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei na Rais Masoud Pezeshkian wameapa kulipiza kisasi cha damu ya Shahidi Haniya.../