Iran yakosoa ripoti ya Ban kuhusu mapatano ya nyuklia
Iran imesema ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Tehran inavyotekeleza mapatano ya nyuklia imejaa maelezo ambayo hayajakamilika.
Ripoti hiyo ya Ban Ki-moon imedai kuwa, hatua ya Iran kufanya majaribio ya makombora ya balistiki ni 'jambo linalokiuka moyo' wa mapatano ya nyuklia ambayo yanajulikana rasmi kama 'Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezwaji (JCPOA)'.
Ripoti hiyo imeitaka Iran isitishe majaribio ya makombora ya balistiki kwa madai kuwa majaribio hayo yanweza kuzidisha wasiwasi katika eneo la Mashariki ya Kati.
Akitoa kauli kufuatia ripoti hiyo, Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran Mohammad Javad Zarif amesema, "Ripoti hiyo imetayarishwa kwa kutegemea taarifa ambazo si kamili na inayonyesha jinsi Katibu Mkuu wa UN asivyoelewa mazungumzo ya nyuklia."
Iran na nchi za 5+1 ambazo ni Russia, China, Ufaransa, Uingereza na Marekani pamoja na Ujerumani zilitiliana saini mapatano ya nyuklia Julai 14 mwaka jana na kuanza kuyatekleza Januari 16 mwaka huu. Zarif amesema pande mbili zilifanya mazungumzo ya miezi 23 mfululizo kabla ya kufikai mwufaka.
"Tumeshasema kabla kuwa, Umoja wa Mataifa haukuwa na nafasi katika kuandika mapatano ya JCPOA, kwa hivyo, kama tunavyoona, kile alichofanya, (Katibu Mkuu wa UN) hakina faida kwa mapatano," ameongeza Zarif.
Iran imesisitiza mara kadhaa kuwa maudhui ya mpango wake wa kujihami, hasa makombora, haiko hata kidogo katika mapatano ya nyuklia.
Aidha Iran inasisitiza kuwa, makombora yake ya balistiki hayana vichwa vya nyuklia kwani nchi hii inapinga umilizi wa silaha za nyuklia.