Abu Sharif: Irada ya muqawama ina nguvu kuliko njama yoyote
Mwakilishi wa Harakati ya Jihad Islami ya Palestina amesema baada ya utawalal wa Kizayuni kumuua shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon kwamba: Licha ya kuipoteza nembo hiyo adhimu, lakini si tu muqawama hautadhoofishwa bali utaendeleza njia yake kwa nguvu zaidi na kwa azma kamili.
Nasser Abu Sharif Mwakilishi wa harakati ya Jihad Islami ya Palestina mjini Tehran ameashiria jinai na mashambulilzi mtawalia ya utawala wa Kizayuni huko Lebanon na kusema: Jinai zinazofanywa na utawala huo ghasibu zinatekelezwa kwa uungaji mkono kamili wa Marekani ili kuyumbisha amani ya Lebanon na kudhoofisha muqawama; na Marekani ndiyo mshirika mkuu wa jinai zote unazozifanya dhidi ya taifa la Lebanon.
Kuhusu kuuliwa shahidi Sayyid Hassan Nasrullah Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon, Abu Sharif amesema: Bila shaka muqawama hautadhoofishwa kwa kuuliwa makamanda wake, lakini irada ya muqawama ina nguvu zaidi kuliko njama yoyote ile, na uchokozi wa Wazayuni hauwezi kulizuia taifa la Lebanon na muqawama katika njia yake.
Baada ya takriban mwaka mmoja wa jinai na vita vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza, kuanzia tarehe 23 mwezi huu wa Septemba, utawala wa Kizayuni umepanua jinai zake hadi Lebanon; na katika jinai yake ya karibuni Ijumaa tarehe 27 Septemba ulikishambulia kitongoji cha Dhahiya kusini mwa Beirut kwa kutumia mabomu mazito uliyopewa na Marekani na kumuuwa shahidi Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah.
Wizara ya Afya ya Lebanon imetangaza kuwa watu zaidi ya 800 wameuawa shahidi na takriban elfu 3 wamejeruhiwa tangu tarehe 23 mwezi huu kutokana na mashambulizi makubwa ya jeshi la utawala katili wa srael huko Lebanon.