Sisitizo la Iran la kuweko mshikamano wa Kiislamu dhidi ya Israel
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza juu ya ulazima wa kuweko umoja na mshikamano wa Waislamu dhidi ya utawala mtendaji jinai na dhalimu wa Kizayuni wa Israel.
Daktari Masoud Pezeshkian amesema hayo mjini Doha alipokutana na Wairani wanaoishi nchini Qatar na kueleza kwamba, kuendelea jinai za kutisha za utawala ghasibu wa Israel kunatokana na kuwepo hitilafu na mirengo kati ya mataifa ya Kiislamu na hivyo ametoa mwito wa kuimarishwa umoja wao dhidi ya utawala wa Kizayuni.
Rais wa Iran Waislamu amebainisha kwamba, kama Waislamu watauungana na kuwa kitu kimoja, watajiletea izza na heshima, na hakuna atakayethubutu kuwatazama kwa jicho la dharau au vitisho.
THapana shaka kuwa, takwa hili ni muhimu kwa sababu jamii na mataifa ya Kiislamu yana mambo mengi yanayofanana na wanayoshirikiana baina yao kwa ajili ya kuimarisha uhusiano baina yao na kuunda Umma wa kweli wa Kiislamu, ambapo kama hili litazingatiwa na kufanyiwa kazi, Waislamu watakuwa wamefanikiwa kuunda asasi yenye nguvu zaidi kuliko Umoja wa Ulaya.

Kwa mujibu wa mafundisho matukufu ya Uislamu, Qur’ani ni kitabu kikubwa zaidi cha Mwenyezi Mungu ambacho Waislamu wote wanashirikiana katika hilo na kinasisitiza umoja wa Waislamu dhidi ya makafiri na maadui zao. Aidha, Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) ndiye mjumbe wa mwisho wa Mwenyezi Mungu kwa walimwengu, Mtume ambaye ni wa Waislamu wote na ambaye mazungumzo yake na tabia yake katika kukabiliana na maadui ni ruwaza na mfano mzuri sana kwa zama za sasa kwa umoja na udugu wa Waislamu dhidi ya maadui zao.
Mbali na masuala ya kidini, Waislamu pia wanakabiliwa na changamoto za pamoja katika masuala ya usalama, kama vile jinai za utawala ghasibu wa Kizayuni na kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina, jambo ambalo pia linaonesha haja na ulazima wa kuimarishwa mshikamano na umoja baina ya nchi za Kiislamu.
Umoja wa mshikamano baina ya mataifa ya Kiislamu ni jambo ambalo limekuwa likitiliwa mkazo mno na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama wenzo wa kuweza kukabiliana nan maadui. Suala jingine ambalo nalo limekuwa likipigiwa upatu na Iran ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano wake na majirani zake.

Katika miaka ya hivi karibuni, serikali zilizoingia madarakani nchini Iran husuasn serikali iliyopita ya shahidi Ebrahim Raisi sera hii ilidhihirika na kuonekana zaidi na hata serikali ya sasa ya Rais Masoud Pezeshkian imesisitiza mara kadhaa juu ya kuendeleza njia hii katika sera zake za kigeni.
Kilicho muhimu kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hususan katika hali ilivyo hivi sasa ni kutekelezwa kivitendo makubaliano ya kuimarisha mafungamano na umoja baina ya nchi za Kiislamu, ili maadui wa Waislamu wajue kwamba mazungumzo ya kuimarisha mafungamano na umoja hayaishii tu katika makaratasi na viongozi wa jamii ya Kiislamu kwa kuelewa na kuduriki hali ilivyo hivi sasa ambapo utawala ghasibu wa Kizayuni unaendelea kuwaua Waislamu wa Gaza na Lebanon, wameungana na kwa kuunganisha uwezo wao wote, wameamua kukabiliana na adui wa Waislamu ili kuushinda utawala huu unaoakalia kwa mabavu ardhi za Palestina.