Iran yakanusha tuhuma za uongo kwamba Tehran inaingilia uchaguzi wa Marekani
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amekanusha tuhuma zinazodai kuwa Iran inaingilia uchaguzi wa rais wa Marekani, na kusema serikali ya nchi hiyo haina mamlaka ya kutoa tuhuma kama hizo.
Akijibu ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani na baadhi ya tuhuma kuhusu eti uingiliaji wa Iran katika uchaguzi wa nchi hiyo, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmaeil Baghaei amesisitiza kuwa: Serikali ya Marekani ambayo ina historia ndefu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kinyume cha sheria, haina hadhi ya kutoa tuhuma kama hizo dhidi ya nchi nyingine.
Esmaeil Baghaei amesema ripoti ya kila mwaka ya Wizara ya Usalama wa Ndani ya Marekani inayodai kuwa baadhi ya nchi, ikiwemo Iran, zinatumia akili mnemba (artificial intelligence) kueneza habari za uwongo au za kuzusha mgawanyiko kuhusu uchaguzi wa rais wa Marekani, haina msingi wowote.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: Madai hayo ya kukaririwa na yasiyo na msingi ambayo yamekuwa yakitolewa na baadhi ya viongozi na taasisi za Marekani kwa muda mrefu, yamechochewa na matamshi ya kisiasa kwa ajili ya matumizi ya ndani.

Baghaei amesisitiza kuwa, serikali ya Marekani ambayo ina historia ndefu ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine kinyume cha sheria, haina hadhi na mamlaka ya kunasibisha tuhuma hizo kwa nchi nyingine.
Uchaguzi wa rais wa Marekani utafanyika Novemba mwaka huu, na wagombea wa nafasi hiyo wanatumia mbinu na propaganda za aina zote ili kuvutia kura nyingi, ikiwa ni pamoja ya kuzituhumu nchi nyingine.