Spika: Mauaji ya kigaidi kuharakisha kuporomoka utawala wa Kizayuni
(last modified Fri, 11 Oct 2024 10:32:06 GMT )
Oct 11, 2024 10:32 UTC
  • Spika: Mauaji ya kigaidi kuharakisha kuporomoka utawala wa Kizayuni

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) amesema kuwa, mashambulizi ya anga na mauaji ya kigaidi yanayofanywa na utawala haramu wa Israel hayatakuwa na matokeo mengine isipokuwa kuharakisha kusambaratika na kuangamia kwa utawala huo wa Kizayuni.

Mohammad Bagher Ghalibaf amesema hayo akihutubia kongamano la kimataifa la maadhimisho ya miaka 30 ya Katiba ya Jamhuri ya Tajikistan mjini Dushanbe na kusisitiza kuwa, kuna haja ya kutia saini mkataba wa muungano wa mabunge ya nchi za eneo hili.

Spika wa Bunge la Iran amesema, utawala wa Kizayuni lazima ujue kwamba hauwezi kufidia kushindwa kwake kistratijia kwa mashambulizi ya anga na mauaji ya kiholela na kuongeza kuwa, ukatili wa utawala huo unaharakisha tu kuangamia kwake.

Sanjari na kutoa salamu za rambirambi kwa taifa na serikali ya Lebanon kufuatia kuuawa shahidi aliyekuwa Katibu Mkuu wa Harakati ya Mapambano ya Hizbullah, Sayyid Hassan Nasrullah, Ghalibaf amesema kuwa, jinai na vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni katika mwaka mmoja uliopita ni ishara tosha ya kushindwa utawala huo kukabiliana na mataifa shupavu ya Palestina na Lebanon.

Katika ziara yake ya Tajikistan, Spika wa Bunge la Iran amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa ngazi za juu wa nchi hiyo akiwemo Rais Emomali Rahmon, Mwenyekiti wa Bunge la Kitaifa Rustam Emomali, na Spika wa Baraza la Wawakilishi, Mohammad Taher Zakerzadeh.

Tags