Araghchi: Kuuawa Mujahidina wa Njia ya Haki hakutavunja Kambi ya Muqawama
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imetoa salamu za rambirambi kufuatia mauaji ya Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Hamas.
Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran imesisitiza kuwa, kuuawa Mujahidina wanaopigana katika njia ya heshima na utu wa binadamu, si tu kwamba hakutii dosari katika fikra na njia ya Muqawama na mapambano ya ukombozi, bali kifo chao kitukufu ni msisitizo juu ya haki na usahihi wa njia yao na kinatoa msukumo na kuwahamasisha wafuasi wa njia hiyo na Mujahidina katika njia ya kupigania izza na uhuru.
Taarifa hiyo imetolewa baada ya harakati ya Hamas kuthibitisha kuwa, Yahya Sinwar, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina, ameungana na wenzake waliouawa shahidi wakipambana na adui, yaani utawala ghasibu wa Israel, katika mji wa Rafah (kusini mwa Ukanda wa Gaza) siku ya Jumatano.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani jinai ya utawala wa Kizayuni ya kuwaua kigaidi viongozi na shakhsia wa Palestina na kutangaza kuwa, Marekani ni mshirika katika kutekeleza jinai hizo na inawajibika kwa kutoa silaha na kuuhami kifedha na kisiasa utawala huo.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza kuwa, jina la Sinwar limewekwa katika kitabu cha mashujaa wakubwa wa Umma wa Kiislamu kama Sheikh Ahmad Yassin, Abdul Aziz Rantisi, Qassem Soleimani, Ismail Haniyeh na Sayyid Hassan Nasrullah, ambao wamesabilia uhai wao wote katika njia ya Muqawama na Jihadi kwa ajili ya kukomesha uvamizi na kutimiza haki ya kisheria na halali ya kujitawala na haki ya kimsingi ya kuishi kwa heshima.

Wakati huo huo, Sayyid Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia amesema: Yahya Sinwar hakuogopa kifo, bali alikuwa akitafuta daraja ya juu ya kuuliwa shahidi huko Gaza; Alipigana kwa ujasiri kwenye uwanja wa vita hadi pumzi yake ya mwisho.