IRGC: Vipigo vya kushtukiza na kushangaza vinaisubiri Israel
(last modified Wed, 30 Oct 2024 03:29:55 GMT )
Oct 30, 2024 03:29 UTC
  • IRGC: Vipigo vya kushtukiza na kushangaza vinaisubiri Israel

Kamanda wa ngazi za juu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) ameonya kwamba, mipango mipya ya majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu itaishangaza Israel katika siku zijazo na kusisitiza kuwa, utawala huo wa kihalifu utakabiliana na hali mbaya zaidi kutokana na vipigo kutoka taifa hili.

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi, Naibu Kamanda wa Uratibu wa IRGC aliyasema hayo jana Jumanne, siku tatu baada ya Israel kufanya shambulio la kichokozi dhidi ya vituo vya kijeshi vya Iran, ambalo Iran imeapa kujibu.

Uvamizi huo wa kigaidi ulikuja wakati huu ambapo utawala huo unaoikalia kwa mabavu Palestina ukiwa umezama katika kinamasi cha vita vyake vya umwagaji damu katika Ukanda wa Gaza na Lebanon.

Naibu Kamanda wa Uratibu wa SEPAH ameeleza bayana kuwa, "Katika siku zijazo, utawala wa Kizayuni utapokea mapigo makubwa zaidi, ya kushangaza na ya kushtukiza." 

Makombora ya balestiki ya Iran

Brigedia Jenerali Mohammad Reza Naqdi pia amebainisha kuwa, Muqawama huko Gaza na Lebanon umepunguza kiburi cha madola ya kibeberu katika medani ya kimataifa.

Ameeleza bayana kuwa, aina ya uungaji mkono kwa Israel hivi sasa ni tofauti na ule uliokuwa ukitolewa na washirika na waungaji mkono wa utawala huo pandikizi, kutokana na kusimama kidete mrengo wa Muqawama.