Iran: Tutajibu iwapo Israel itarusha hata mshale jangwani
(last modified Thu, 31 Oct 2024 02:37:36 GMT )
Oct 31, 2024 02:37 UTC
  • Iran: Tutajibu iwapo Israel itarusha hata mshale jangwani

Vyombo vya ulinzi vya Iran vimesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itajibu mapigo ya uchokozi wowote wa Israel dhidi ya ardhi yake, hata kama hatua hiyo ni ndogo na isiyo na tija, kama kurusha mshale kuelekea kwenye jangwa moja la nchi hii.

Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari pambizoni mwa kikao cha Baraza la Mawaziri Jumatano ya jana.

Amesisitiza kuwa, "Hata kama utawala wa Kizayuni utarusha mshale kuilenga nchi yetu, Iran haitaisamehe, na bila shaka itawajibu Wazayuni."

Akiashiria mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala wa kigaidi wa Israel dhidi ya Iran mapema wiki hii, Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema kuwa, hakuna ndege ya kivita iliyoingia katika anga ya nchi hii wakati wa uvamizi na uchokozi huo wa Wazayuni.

Kadhalika Brigedia Jenerali Nasirzadeh ameeleza bayana kuwa, "Hakuna tatizo lililofanywa katika mchakato wa utengenezaji wa makombora."

Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Aziz Nasirzadeh

Kikosi cha Ulinzi wa Anga ya Iran kilisema katika taarifa yake Jumamosi kwamba, mfumo wa ulinzi wa anga wa nchi hii ulifanikiwa kukabiliana na shambulio hilo la kichokozi la Israel.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu haitaki vita, lakini haitafumbia macho haki yake ya kutoa jibu linalostahiki kwa uchokozi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

 

Tags