Iran yalihimiza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lisimamishe uwanachama wa Israel
(last modified Thu, 07 Nov 2024 03:31:23 GMT )
Nov 07, 2024 03:31 UTC
  • Iran yalihimiza Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lisimamishe uwanachama wa Israel

Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa amelihimiza Baraza Kuu la umoja huo lisimamishe uwanachama wa utawala ghasibu wa Israel kutokana na jinai unazoendelea kufanya dhidi ya Wapalestina, ikiwa ni pamoja na kupiga marufuku shughuli za shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi wa Kipalestina.

Amir Saeid Iravani ameyasema hayo mapema leo kabla ya mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kusikiliza taarifa fupi kuhusu Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA.
 
Iravani amesisitiza kwa kusema: "Iran inatoa wito kwa jamii ya kimataifa kuchukua hatua kali kujibu hatua za Israel na kusimamisha uwanachama wa Israel katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kutokana na ukiukaji wake wa wazi wa Hati ya Umoja wa Mataifa na sheria za kimataifa".
 
Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ametoa mfano wa tangazo lililotolewa siku ya Jumatatu na utawala huo la kuufahamisha Umoja wa Mataifa kwamba umeamua kupiga marufuku shughuli za UNRWA, hatua ambayo itahitimisha kazi muhimu sana inayofanywa na shirika hilo kwa miongo kadhaa sasa ya kupeleka misaada muhimu katika maeneo ya Palestina na hivyo kuyaweka hatarini maisha ya mamilioni ya Wapalestina.
Unyama unaofanywa na Israel Ghaza haumithiliki wala hauelezeki 

Iravani amelaani hatua hiyo akisema ni jaribio la kuwanyima Wapalestina huduma muhimu kama vile elimu, afya na misaada ya kibinadamu.

 
Kadhalika, balozi huyo ameashiria vita vya mauaji ya kimbari vilivyoanzishwa mwezi Oktoba 2023 na utawala huo haramu katika Ukanda wa Ghaza, vikiwa hadi sasa vimeshaua karibu Wapalestina 43,400, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, na jinai nyingine za kivita na jinai dhidi ya binadamu ulizofanya dhidi ya Wapalestina.

Iravani amebainisha kuwa, vitendo vya utawala wa Kizayuni sio ni kielelezo cha ukikwaji mkubwa wa haki za binadamu, lakini pia hatua yake ya kuitumia njaa makusudi kama silaha, inzidisha hali mbaya ya kibinadamu na kuandaa mazingira yasiyoweza kuvumilika kwa watu wa Palestina.

Amesisitiza kuwa hatua hizo zinatoa tishio la moja kwa moja kwa amani na usalama wa kimataifa na kwa sababu hiyo kuna ulazima wa kuuwajibisha utawala ghasibu wa Israel kwa matendo yake.../