Rais Pezeshkian: Iran inapigania usalama na amani duniani
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba ulimwengu unaelewa kuwa Iran inafuatilia amani na usalama duniani kote na kwamba, mpango wake wa nyuklia ni wa malengo ya amani.
Rais Pezeshkian amesema hayo katika mazungumzo yake na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kubainisha wazi kwamba, "Iran haifuatilii kutengeneza silaha za nyuklia, na huu ni msimamo usiobadilika wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Aidha Pezeshkian amesema katika mazungumzo yake hayo na Grossi kwamba, mpango wa nyuklia wa Iran unafanyika kwa mujibu wa mfumo wa kisheria wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kwamba, Iran inatarajia haki zake zitazingatiwa na kuheshimiwa na wakala huo kama ilivyo kwa nchi zingine.
Kadhalika amesema, Iran iko tayari kushirikiana na IAEA kutatua kile kinachoonekana kama utata kuhusu mpango wake wa amani wa nyuklia.
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA aliwasili Tehran juzi Jumatano akiongoza ujumbe wa wakala huo kwa lengo la kuzungumza na viongozi wakuu wa masuala ya nyuklia na kisiasa wa Iran.