Iran yasisitiza kutekelezwa haraka na kikamilifu hati ya kuwakamata Netanyahu na Gallant
(last modified Tue, 26 Nov 2024 08:04:39 GMT )
Nov 26, 2024 08:04 UTC

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi amesisitiza kutekelezwa haraka na kikamilifu hati iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ya kuwatia nguvuni Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant, waziri mkuu na waziri wa zamani wa vita wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Araghchi, ametoa sisitizo hilo katika mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Kundi la Marafiki Watetezi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa uliofanyika kupitia mawasiliano ya video, ambapo sambamba na kubainisha kuwa, kutolewa waranti wa kuwakamata Netanyahu na Gallant na Mahakama ya ICC ni hatua moja ya kufikiwa haki na kuwawajibisha wahalifu wa Kizayuni, amesema: "kutekelezwa haraka na kikamilifu hati hii ndilo takwa la wote katika ngazi ya kimataifa".
 
Katika mkutano huo, ambao umefanyika kwa ubunifu na kwa pendekezo la Iran ili kubadilishana mawazo kuhusu matukio ya Asia Magharibi yaliyotokana na jinai za utawala wa Kizayuni, Araghchi amekaribisha hati iliyotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai na akasema, jamii ya kimataifa ina wajibu wa kuchukua hatua ya kuzuia muelekeo wa kuufanya uonekane jambo la kawaida uhalifu na jinai za kinyama na mauaji ya kimbari unayofanya utawala wa Kizayuni huko Palestina.
 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameongeza kuwa, kutolewa hati ya kukamatwa Netanyahu na Gallant na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ni hatua inayotia matumaini ya kupatikana haki na kuwawajibisha wahalifu wa Kizayuni kwa mauaji ya kimbari, jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu walizofanya.

Kadhalika, Araghchi amebainisha kuwa, jamii ya kimataifa inapaswa kuwakemea na kuwawajibisha pia wasaidizi na waungaji mkono wa utawala wa Kizayuni hususan Marekani. Amesema, wao ni washirika katika mauaji ya kimbari na jinai za kivita za utawala huo ghasibu, kwa sababu wanatoa silaha hatari za kuwaulia Wapalestina wasio na hatia na kukwamisha hatua yoyote ya maana inayotaka kuchukuliwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kusimamisha jinai za utawala wa Kizayuni.

 
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza pia kwa kusema: "hatutaruhusu hali ya sasa ya Palestina na unyama unaofanywa na utawala unaoikalia Quds kwa mabavu liwe jambo la kawaida".
 
Siku ya Alkhamisi, tarehe 21 Novemba, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa hati ya kukamatwa viongozi wa Kizayuni Benjamin Netanyahu na Yoav Galant, hatua ambayo imekaribishwa na jamii ya kimataifa.../