Pezeshkian ampongeza Rais mpya wa Lebanon; asisitiza umoja na kuimarisha utulivu
(last modified Sat, 11 Jan 2025 02:58:15 GMT )
Jan 11, 2025 02:58 UTC
  • Pezeshkian ampongeza Rais mpya wa Lebanon; asisitiza umoja na kuimarisha utulivu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia ujumbe Rais mpya wa Lebanon na kusisitiza kuwa umoja na kuimarisha utulivu vitazima njama za kujitanua na tamaa za adui Mzayuni dhidi ya Lebanon.

Rais Masoud Pezeshkian jana Ijumaa alimtumia ujumbe Jenerali Joseph Aoun na kumpongeza kwa kuchaguliwa kuwa Rais mpya wa Lebanon kufuatia kura nyingi za wawakilishi wa Bunge la nchi hiyo.

Rais Pezeshkian amesema anataraji kuwa uchaguzi huu ambao ni matokeo ya mapatano ya vyama na makundi mengi ya kisiasa nchini Lebanon, utaimarisha utulivu wa kisiasa, ustawi wa uchumi na maendeleo, amani na faraja kwa wananchi azizi wa Lebanon.  

Jenerali Joseph Aoun alichaguliwa juzi Alkhamisi kuwa Rais wa Lebanon kwa kura 99 za 'ndiyo' katika bunge lenye viti 128 la Lebanon. 

Joseph Aoun

Hii ni mara ya tano katika historia ya Lebanon kwa kamanda wa jeshi kuwa rais wa nchi.

Kuchaguliwa Joseph Aoun kuwa rais mpya wa Lebanon kunahitimisha ombwe la muda mrefu la uongozi ambalo lilikuwa limezuia mageuzi muhimu na kuzidisha hofu ya kuporomoka zaidi nchi hiyo inayosumbuliwa na migogoro mingi ya kitaifa.