Iran yakanusha tuhuma za Israel za kupeleka silaha Lebanon
(last modified Sat, 25 Jan 2025 11:35:54 GMT )
Jan 25, 2025 11:35 UTC
  • Iran yakanusha tuhuma za Israel za kupeleka silaha Lebanon

Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa amepuuzilia mbali madai ya Israel kamba Jamhuri ya Kiislamu inasafirisha kimagendo silaha kwenda Lebanon.

Katika taarifa, Amir Saeid Iravani, Balozi wa Iran katika Umoja wa Mataifa ameeleza kuwa, "Madai hayo hayana jingine isipokuwa kujaribu kuhalalisha hatua ya kukaririwa ya utawala wa Israel ya kukanyaga Azimio Nambari 1701 (2006) la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa."

Iravani ameongeza kuwa, lengo jingine la utawala wa Kizayuni kuibua madai hayo ni kuhalalisha hatua ya Tel Aviv ya kutoheshimu makubaliano ya usitishaji vita kati yake na Lebanon. 

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran amebainisha kuwa: "Utawala huu hauna nia ya kuzingatia ahadi zake za kujiondoa kutoka kusini mwa Lebanon baada ya muda wa siku 60 wa kusitisha mapigano, kwa mujibu wa masharti yaliyowekwa. Badala yake, utawala ghasibu wa Israel unaibua tuhuma hizo zisizo na msingi ili kuhalalisha uvamizi wake haramu unaoendelea katika ardhi ya Lebanon."

Wanamuqawama wa Hizbullah ya Lebanon

Iravani amesema Baraza la Usalama ni lazima liulazimishe utawala wa Israel kutekeleza kikamilifu wajibu wake chini ya mpango wa usitishaji vita, usitishe mara moja ukiukaji wake dhidi ya mamlaka ya kujitawala na ardhi ya Lebanon, na uondoe vikosi vyake kutoka kusini mwa Lebanon bila kuchelewa.

Haya yanajiri huku vyombo vya habari vya Kiebrania vikiripoti kuwa, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel halitaondoka kusini mwa Lebanon utakapomalizika muhula uliowekwa wa siku 60 kesho Jumapili kulingana na makubaliano ya kusitisha vita yaliyofikiwa kati ya Israel na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Lebanon ya Hizbullah.