Spika Qalibaf: Hamas ipo hai, imeidhalilisha vibaya Israel
Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran) ameipongeza Harakati ya Muqawama ya Hamas na vikosi vya mapambano ya Kiislamu vya Palestina kwa ushindi wao mkabala wa utawala wa Kizayuni.
Mohammad Baqer Qalibaf ameipongeza Hamas na vikosi vingine vya Muqawama katika eneo zima kuibuka washindi dhidi ya Israel na kusisitiza kuwa, utawala huo wa Kizayuni umeshindwa katika majaribio yake ya kueneza dhana ya kuwa umeshinda Mhimili wa Muqawama.
Akihutubia kikao cha Bunge leo Jumatatu, Qalibaf ameashiria kushindwa kwa 'vita vya utambuzi' vya utawala ghasibu wa Israel na kushindwa majaribio yake ya kueneza dhana potofu kwamba wavamizi hao wameushinda Muqawama huko Palestina na Lebanon.
Spika Qalibaf amesisitiza kuwa, “Imedhihirika leo kwamba Hamas iko hai na inashamiri. Muqawama unaendelea kwa azma yenye nguvu zaidi kuliko hapo awali na unamdhalilisha adui,”
Ameeleza kuwa, uvumilivu wa Palestina mbele ya jinai za mauaji ya kimbari za Israel zilizodumu kwa zaidi ya miezi 15, utakamiika baada ya Wazayuni kuondoka kikamilifu katika Ukanda wa Gaza, na kurejea mwakao Wapalestina waliokimbia makazi yao.
Qalibaf pia ametoa pongezi kwa Mashahidi wa Muqawama, akiwemo aliyekuwa Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas, Ismail Haniyah, kiongozi wa Hamas Yahya Sinwar, Katibu Mkuu wa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon, Sayyid Hassan Nasrullah, Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Hizbullah, Hashem Safieddine, na wale wote waliosabilia maisha yao katika vita vitakatifu dhidi ya utawala wa Kizayuni, ambaye ndiye adui mbaya zaidi wa binadamu.