Velayati: Iran, Uturuki zina nafasi chanya katika ulimwengu wa Kiislamu
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i12367-velayati_iran_uturuki_zina_nafasi_chanya_katika_ulimwengu_wa_kiislamu
Mshauri wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zina nafasi muhimu katika kuboresha mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu.
(last modified 2025-12-03T16:38:35+00:00 )
Aug 01, 2016 04:04 UTC
  • Velayati: Iran, Uturuki zina nafasi chanya katika ulimwengu wa Kiislamu

Mshauri wa Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki zina nafasi muhimu katika kuboresha mustakabali wa ulimwengu wa Kiislamu.

Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa aliyasema hayo jana Jumapili katika mazungumzo yake na Riza Hakan Tekin, Balozi wa Uturuki mjini Tehran na kusisitiza kuwa, nchi mbili hizi ni muhimu sana katika kuainisha na kuboresha mustakabali wa nchi za Kiislamu sambamba na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zinazozikabili.

Ali Akbar Velayati, Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa

Kadhalika Velayati amewapongeza wananchi wa Uturuki kwa kuzima jaribio la mapinduzi ya kijeshi la hivi karibuni na kusisitiza kuwa taifa la Iran lilisimama wakati huo na linaendelea kusimama na serikali na taifa la Uturuki dhidi ya njama hizo za maadui. Watu karibu 300 waliuawa na wengine zaidi ya 2,000 kujeruhiwa katika tukio hilo la Julai 15.

Mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika Masuala ya Kimataifa ameongeza kuwa, lengo la Iran ni kuimarisha uhusiano na ushirikiano na Uturuki katika nyuga tofauti licha ya tofauti zao za kimitazamo.

Mapinduzi ya kijeshi yaliyofeli Uturuki

Kwa upande wake, Riza Hakan Tekin, Balozi wa Uturuki hapa nchini ameipongeza Iran kwa kusimama na taifa lake wakati wa kujiri tukio hilo alilolitaja kuwa la kuhuzunisha na kuashiria kuwa, uhusiano wa Tehran na Ankara kwa sasa umefikia upeo wa juu katika kipindi cha miaka 10 iliyopita.