Iran: Haitatokea katu kufanywa mazungumzo ya kuufumua mpango wetu wa nyuklia
Mar 10, 2025 03:08 UTC
Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu wa Iran katika Umoja wa Mataifa imetangaza kwamba ikiwa lengo la kutaka kufanya mazungumzo na Jamhuri ya Kiislamu ni "kuufumua mpango wa amani wa nyuklia wa Iran," mazungumzo kama hayo hayatafanyika katu.
Katika taarifa ya mjibizo iliyotoa kujibu tamko la serikali mpya wa Marekani kwamba iko tayari kufanya mazungumzo na Iran, Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa imeandika kwenye mtandao wa kijamii wa X: "ikiwa madhumuni ya mazungumzo hayo ni kufikia lengo la kuondoa wasiwasi kuhusu uwezekano wa mpango wa nyuklia wa Iran kuwa wa malengo ya kijeshi, hilo linaweza kufanyika; lakini kama madhumuni yatakuwa ni kuufumua mpango wa amani wa nyuklia wa Iran, yaani serikali ya Trump kutaka kufanya kile ambacho Obama alishindw kukifanya, mazungumzo kama hayo hayatafanyika kamwe".
Iran imeshatangaza mara kadhaa kwamba hakutakuwa na mazungumzo na Marekani chini ya vikwazo na mashinikizo ya juu kabisa.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza siku ya Ijumaa alipozungumza mbele ya waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, kwamba amemtumia barua Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kusema: "kutakuwa na siku za kuvutia huko tunakoelekea, ni hilo tu ndilo ninaloweza kukuambieni".
Rais wa Marekani aliongezea kwa kusema: "huu ni wakati wa kuvutia katika historia ya dunia, sisi na Iran tuko kwenye hali, ambapo muda mfupi sana ujao litajiri tukio fulani. Tunatumai kwamba tutaweza kufikia kwenye mkataba wa amani. Sizungumzi kutokana na nguvu au udhaifu. Nasema tu ningependelea kuona mapatano ya amani kuliko (chaguo) jengine. Lakini (ikishindikana,chaguo) jingine litatatua tatizo"../
Tags