Iran inafuatilia malengo gani katika kupanua uhusiano na nchi za Afrika?
Kikao cha kubadilishana mawazo cha Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano wa Kiuchumi wa Iran na Afrika kimefanyika mjini Tehran, kwa uratibu wa Shirika la Maendeleo ya Biashara, kikihudhuriwa na mabalozi na wawakilishi wa nchi za Afrika.
Mohammad Ali Dehghan Dehnavi, mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Biashara la Iran amesema katika kikao hicho kwamba: Mkutano wa Tatu wa Ushirikiano kati ya Iran na Afrika utafanyika katika muda wa miezi miwili ijayo. Akigusia umuhimu wa kustawishwa kistratijia uhusiano kati ya Iran na Afrika katika Serikali ya Awamu ya 14, Dehghan Dehnavi ameongeza kuwa: Shirika la Maendeleo ya Biashara lina zana mbalimbali za kuendeleza uhusiano na Afrika ikiwa ni pamoja na kufanya maonesho mbalimbali, kutuma na kupokea wajumbe wa kibiashara na kufanya mazungumzo rasmi na mamlaka za nchi.
Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Biashara amesisitiza kuwa: Mazungumzo ya shirika hilo na sekta binafsi katika bara la Afrika yanaonyesha kuwa sekta hizi zina nia kubwa ya kuwekeza barani humo. Dehghan Dehnavi amesema: Ili kuongeza mabadilishano ya biashara, imeamuliwa kuanzisha safari za meli kuelekea Afrika Magharibi.

Katika miaka ya hivi karibuni, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetekeleza mipango mingi na mbalimbali ya kupanua ushirikiano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni na nchi za Kiafrika. Mikutano ya pande mbili na ya pande nyingi ya maafisa wa Iran na wenzao wa nchi za Kiafrika, kufanya maonyesho ya pamoja ya kutambulisha uwezo wa kiuchumi wa makampuni ya umma na ya kibinafsi ya Iran, na vilevile kuwekeza katika miundombinu ya kiuchumi na ya kiafya ya nchi kadhaa za Kiafrika ni miongoni mwa mipango na malengo ambayo Iran imefuatilia na kutekeleza katika bara hilo kubwa.
Kwa kuzingatia eneo kubwa la mwambao wa Iran, na vifaa vya kipekee vya bandari kusini mwa nchi, pamoja na bandari ya Chabahar (kusini-mashariki mwa Iran), kuna uwezo mkubwa na muhimu wa kutuma bidhaa kutoka Iran hadi bara la Afrika. Kwa upande mwingine, nchi za Kiafrika pia zinaweza kutumia suhula na uwezo wa kiuchumi wa Iran.
Mbali na ukweli kwamba bara la Afrika lina rasilimali nyingi za asili na linaweza kuwa mshirika mzuri wa Iran kwa mtazamo wa kiuchumi, pia linawezo kuwa nafasi muhimu kisiasa katika kuiunga mkono Iran katika asasi za kikanda na kimataifa, jambo ambalo linaweza kufikiwa kwa kutilia maanani masuala yanayozikutanisha pamoja pande hizo mbili.
Makampuni ya sayansi ya Iran, kutokana na juhudi za wataalamu vijana na wanasayansi wa Iran, yamepata maendeleo makubwa katika miaka ya hivi karibuni, na Iran inaweza kukidhi mahitaji ya kisayansi na maalumu ya nchi za Kiafrika katika nyanja mbalimbali za sayansi na viwanda.
Vilevile, kuanzishwa safari za kawaida za meli, kutayarisha miundombinu inayofaa na kutia saini makubaliano ya kupunguza ushuru wa kibiashara kunaweza kuwa na taathira katika ongezeko la biashara kati ya Iran na bara la Afrika.
Mbali na nyanja za kiuchumi na kibiashara, upande wa kisiasa wa uhusiano na nchi za bara la Afrika pia ni muhimu kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Nchi za Kiafrika zinaunda thuluthi moja ya nchi za dunia, hivyo kupanua uhusiano na nchi hizo kunaweza kujenga misingi imara zaidi ya uungaji mkono wa kimataifa kwa Iran ambayo iko chini ya vikwazo vilivyo kinyume cha sheria vya nchi za Magharibi ikiwemo Marekani.
Kuna nchi 30 za Kiislamu katika bara la Afrika na takriban 50% ya wakazi wake ni Waislamu; Pia, nchi 50 kati ya 54 za bara hilo ni wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa.

Wakati huo huo, inatupasa kutambua kwamba, kuanzishwa safari za meli kati ya Iran na nchi za Afrika kunaweza kuwa chachu ya kustawisha zaidi uhusiano wa kiuchumi kati ya bara hilo na eneo la Magharibi mwa Asia. Uwezo wa Iran katika sekta ya nishati unaweza kudhamini mahitaji yanayoongezeka ya nchi za Kiafrika katika uwanja huu, na kutokana na uanachama wa nchi kadhaa za Kiafrika zikiwemo Algeria, Libya, Nigeria na Angola katika Jumuiya ya Nchi Zinazouza Petroli (OPEC), kuna uwanja mwafaka wa ushirikiano kati ya Iran na nchi hizo.
Alaa kulli hal, duru mpya ya ushirikiano kati ya Iran na nchi za Kiafrika itaegemea zaidi katika uwepo wa sekta binafsi, ambayo pamoja na uwezo wa Iran katika sekta ya uchumi na sayansi ya kisasa, utajenga msingi mwafaka wa uwekezaji katika bara hilo.