National Interest: Mji wa makombora wa Iran unaonyesha nguvu ya nchi hiyo
(last modified Tue, 01 Apr 2025 02:46:09 GMT )
Apr 01, 2025 02:46 UTC
  • National Interest: Mji wa makombora wa Iran unaonyesha nguvu ya nchi hiyo

Gazeti la Marekani la National Interest limeuchambua mji mpya wa makombora wa Iran na kusisitiza kwamba, kufichuliwa mji huo huku hali ya wasiwasi ikiongezeka katika Bahari Nyekundu na Asia Magharibi, ni ujumbe kwa Marekani na maadui wa Iran.National Interest imekiri katika ripoti yake kwamba hifadhi ya makombora ya Iran imeongezeka kwa kiasi kikubwa katika muongo mmoja uliopita.

Tarehe 25 Machi mwaka huu, Jamhuri ya Kiislamu ilizindua mojawapo ya miji yake mipya ya chini ya ardhi ya makombora na kusambaza video yake. Kuzinduliwa kwa mji huo kwenye mtandao pia kumepewa mazingatio na watumiaji wa mitandao wa Magharibi. Baadhi ya watumiaji hao wamesisitiza kuwa "Iran iko tayari."

Hapo awali, kamanda wa Kikosi cha Wanaanga cha IRGC, Jenerali Amir Ali Hajizadeh, alisema katika mahojiano kwamba iwapo Iran itazindua mji mmoja wa makombora kila wiki, uzinduzi huo hauwezi kumalizika hata katika kipindi cha miaka miwili.

Jarida la Marekani la National Interest pia limeashiria mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel mwaka jana na kusisitiza kwamba, makombora ya mwendo wa kasi ya Shahab ni tishio kubwa kwa maadui wa Iran kwa sababu silaha hizo zina uwezo wa kupiga masafa marefu zaidi. Jarida hilo pia limeongeza kuwa Iran ina makombora hatari yanayoweza kufika Israel kwa chini ya dakika kumi na tano.

Jarida hili la Marekani limesema kwamba, kwa mujibu wa ripoti ya Taasisi ya Washington ya Sera ya Mashariki ya Karibu, Iran inakadiriwa kuwa na zaidi ya makombora 3,000 ya balistiki. Limeongeza kuwa, pamoja na hayo, Tehran pia ina nguvu kubwa ya makombora ya cruise.