Grossi asisitiza nafasi ya diplomasia katika suala la nyuklia la Iran
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i125288-grossi_asisitiza_nafasi_ya_diplomasia_katika_suala_la_nyuklia_la_iran
Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), aliwasili Tehran Jumatano, Aprili 16, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.
(last modified 2025-04-17T12:43:05+00:00 )
Apr 17, 2025 12:43 UTC
  • Grossi asisitiza nafasi ya diplomasia katika suala la nyuklia la Iran

Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA), aliwasili Tehran Jumatano, Aprili 16, ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Sayyid Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, na Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki la Iran.

Hapo awali, Kazem Gharibabadi, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje, alisema kuwa ziara hiyo inafanyika ndani ya mfumo wa kuendeleza maingiliano na ushirikiano kati ya pande hizo mbili.

Baada ya kukutana na Araqchi, Grossi aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X akisema: "Kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, wakati wa safari yangu ya Tehran iliyofanyika wakati mwafaka, kuna umuhimu." Amesisitiza kuwa: Ushirikiano na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ni muhimu ili kutoa uhakikisho wa kuaminika kuhusu hali ya amani ya mpango wa nyuklia wa Iran katika wakati ambapo diplomasia inahitajika sana.

Kwa upande mwingine, Rafael Grossi alisema katika mahojiano kabla ya safari yake mjini Tehran kuhusu mazungumzo ya Iran na Marekani na nafasi ya IAEA kwamba: "Sisi si sehemu ya mazungumzo ya pande mbili kati ya Mabwana Araghchi na Witkoff, lakini sisi pia tunayafuatilia." Aliongeza kusema kuwa: "Wanajua vyema kwamba ni lazima tutoe maoni yetu juu ya makubaliano yoyote yanayowezekana, kwa sababu tutawajibika kuyathibitisha. Kwa sababu hiyo, tayari tumeanza mijadala isiyo rasmi nao."

Rafael Grossi

Safari ya Grossi mjini Tehran na kukutana kwake na maafisa wa ngazi za juu wa Iran wakati huu inatambuliwa kuwa muhimu. Baada ya mkwamo wa muda mrefu katika mazungumzo ya nyuklia ya JCPOA kwa upande mmoja na baadhi ya hatua zilizochukuliwa na wakala huo, ikiwa ni pamoja na maazimio yaliyotolewa na Bodi ya Magavana ya IAEA yanayoikosoa Iran na kuitaka Tehran kuzidisha ushirikiano na chombo hicho cha udhibiti wa nyuklia, safari hii huenda ikafungua njia katika uga wa ushirikiano kati ya Iran na wakala huo. Wakati huo huo, safari ya Grossi inadhihirisha nia ya shirika hilo kufahamu na kushiriki katika makubaliano yoyote yanayoweza kufikiwa kati ya Iran na Marekani kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya kiraia. Umuhimu wa safari hiyo mjini Tehran unadhihirika zaidi kuliko wakati mwingine wowote kwa kuzingatia matamshi makali yaliyotolewa na maafisa wa Marekani na shutuma kwamba Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia.

Sisitizo la Grossi kuhusu nafasi ya diplomasia katika kusuluhisha suala la nyuklia la Iran limekuja kwa kuzingatia marufuku ya mashambulizi yoyote dhidi ya vituo vya nyuklia vya nchi wanachama wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki, ikiwa ni pamoja na Iran. Maafisa wa serikali ya Marekani, akiwemo Rais Donald Trump, wamekuwa wakikariri katika taarifa zao kwamba machaguo yote dhidi ya Iran, ikiwa ni pamoja na shambulio la kijeshi, yako mezani, wakidhani kwamba kwa njia hiyo wanawezi kuitia woga na wahka Jamhuri ya Kiislamu. Itakumbukwa pia kwamba, katika ziara yake ya awali mjini Tehran mnamo Novemba 2024, Grossi alisisitiza kwamba shambulio dhidi ya vituo vya nyuklia ni kinyume cha sheria na halipaswi kufanywa.

Licha ya madai ya Marekani kwamba inataka kuizuia Iran kupata silaha za nyuklia, shutuma kwamba Iran inajaribu kutengeneza silaha za nyuklia, haijawahi kuthibitishwa na IAEA. Mnamo Novemba 2024, Grossi aliyekuwa akijibu swali kuhusu uwezekano wa Iran kupata bomu la nyuklia alisema: "Hatuna taarifa yoyote inayoonyesha kwamba Iran kwa sasa ina mpango wa kijeshi wa nyuklia." Grossi amekariri kauli kama hii kabla ya safari yake ya sasa mjini Tehran. Katika mahojiano na gazeti la Ufaransa la Le Monde, Rafael Grossi amesema kuwa, makubaliano yoyote kuhusu Iran bila ya kuushirikishwa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) yatakuwa wino tu kwenye karatasi, na amekiri kuwa Iran haina silaha za nyuklia, ingawa ina kile kinachohitajika kutengeneza bomu la atomiki.

Araqchi na Grossi

Hii ni wakati Marekani, sambamba na Israel, kwa miaka mingi imekuwa ikiishutumu Iran kuwa na mpango wa kijeshi wa nyuklia, licha ya kutotoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai hayo, na imetekeleza hatua za kisiasa na vikwazo dhidi ya Jamhuri ya Kiiislamu kwa kisingizio hicho. Hata hivyo, katika hatua inayopingana waziwazi na msimamo wa serikali ya Marekani kuhusu suala hili, jamii ya masuala ya ujasusi ya Marekani, imepinga madai hayo na kukiri katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba Iran haitengenezi silaha za nyuklia. Katika ripoti yake ya hivi karibuni zaidi kuhusu Iran, iliyotolewa Machi 25, 2025, Mkurugenzi wa Ujasusi wa Kitaifa wa Marekani, Tulsi Gabbard alisema: "Jamii ya ujasusi ya Marekani inaendelea kuamini kwamba Iran haitengenezi silaha za nyuklia na kwamba Kiongozi Mkuu wa Iran hajaidhinisha mpango wa silaha za nyuklia ambao aliusimamisha mwaka 2003."