Saudi Arabia, Iran zinasisitiza azma ya kupanua uhusiano wao wa kijeshi
(last modified Fri, 18 Apr 2025 07:28:44 GMT )
Apr 18, 2025 07:28 UTC
  • Saudi Arabia, Iran zinasisitiza azma ya kupanua uhusiano wao wa kijeshi

Iran imesisitiza juu ya utayarifu wake wa kupanua uhusiano wa kijeshi na Saudi Arabia, wakati huu ambapo Waziri wa Ulinzi wa nchi hiyo ya Kiarabu, Mwanamfalme Khalid bin Salman yuko hapa Tehran tangu jana Alkhamisi kujadili usalama katika eneo hili.

Mkuu wa Majeshi ya Iran, Meja Jenerali Mohammad Bagheri alimwambia Mwanamfalme Khalid bin Salman mjini Tehran hiyo jana kwamba, "Mahusiano mazuri kati ya nchi hizi mbili na majeshi yao yatawakatisha tamaa maadui zetu na kuwapa furaha marafiki zetu."

Bagheri ameishukuru Saudi Arabia kwa ushiriki wake kama mwangalizi katika Mazoezi ya Kijeshi ya Bahari ya Hindi (IONS), yanayojulikana kama IMEX 2024. Luteka hiyo katika Bahari ya India imefanywa na Iran, Russia na Oman, kwa kushirikisha wajumbe wa waangalizi kutoka nchi kadhaa, zikiwemo Saudi Arabia, India, Thailand, Pakistan, Qatar na Bangladesh.

"Tangu kusainiwa "Mkataba wa Beijing" mnamo Machi 2023 wa kurejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya vikosi vya kijeshi vya Iran na Saudi Arabia, uhusiano huo umeendelea kuimarika na kustawi," Jenerali Bagheri amesema.

Jenerali Bagheri amepongeza msimamo wa Saudi Arabia kuhusu suala la Palestina na kulaani ukatili wa Israel katika Ukanda wa Gaza, akisema nchi zote za Kiislamu zinahitaji umoja, huruma na msimamo mmoja ili kukabiliana na jinai hizo za utawala wa Kizayuni.

Mwanamfalme Khalid ametoa shukrani zake kwa Jamhuri ya Kiislamu na wakuu wa Majeshi ya Iran kwa mapokezi mazuri aliyopewa pamoja na ujumbe wake mjini Tehran, akisema "ukarimu wenu unaonyesha uhusiano mzuri sana kati yetu."

Amesema uhusiano muhimu kati ya nchi hizi mbili una taathira kubwa katika kuhakikisha usalama wa eneo hili na kuongeza kuwa, Utawala wa Kifalme wa Saudi Arabia unasisitiza juu ya kuimarisha na kuendeleza uhusiano kati ya nchi hizi mbili.

"Mungu akipenda, matokeo ya mahusiano haya mazuri na kuboreka kwao katika nyanja mbalimbali yatakuwa na taathira chanya kwa nchi hizi mbili na eneo kwa ujumla," ameongeza  Waziri wa Ulinzi wa Saudia.