Iran: Sharti la msingi katika mazungumzo yoyote ni kuondolewa vikwazo
Esmail Baghaei, msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kwamba, mahitaji yetu ya kimsingi katika mazungumzo yoyote ni kuondolewa vikwazo kwa njia ambayo italeta matokeo yanayoonekana na yenye ufanisi.
Esmail Baghaei amesema hayo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari siku ya Jumatatu kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliitembelea Russia hivi karibuni, na kufuatiwa na mikutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia, kando ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Marekani.
Aliongeza, "Waziri wa Mambo ya Nje amepanga kufanya ziara rasmi nchini China leo Jumanne.
Kuhusiana na malengo ya mazungumzo yanayoendelea na Marekani, amesema: "Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Iran kimsingi havina uhalali na hatutofautishi kati ya aina moja na nyingine.
Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amebainisha kuwa, tuna uzoefu wa awali na makubaliano ya nyuklia na tunafahamu kikamilifu ukiukaji ambao tumeshuhudia. Kwa hivyo, hitajio letu la msingi katika mazungumzo yoyote ni kuondolewa vikwazo kwa njia ambayo italeta matokeo yanayoonekana na yenye ufanisi.
Duru ya kwanza ya mazungumzo hayo ilifanyika Jumamosi iliyopita Aprili 12 nchini Oman.
Katika duru ya kwanza ya mazungumzo, pande mbili zilikubaliana kwamba msingi wa mazungumzo hayo utakuwa ni "Iran kufanya iaminike na itoe hakikisho kwamba programu yake ya nyuklia ni ya malengo ya amani" na mkabala wake "iondolewe vikwazo na Marekani kwa namna itakayokuwa na taathira".