Mpango wa nyuklia wa Iran, ajenda ya mazungumzo ya pande nne za Iran, China, Russia na Mkuu wa IAEA
(last modified Fri, 25 Apr 2025 03:14:16 GMT )
Apr 25, 2025 03:14 UTC
  • Mpango wa nyuklia wa Iran, ajenda ya mazungumzo ya pande nne za Iran, China, Russia na Mkuu wa IAEA

Wawakilishi wa Iran, China na Russia wamekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kujadili hali ya mpango wa nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.

Balozi wa Russia katika mashirika ya kimataifa yenye makao yake makuu mjini Vienna amesema, jana Alkhamisi Aprili 24 wawakilishi wa Iran, China na Russia walijadili hali ya mpango wa nyuklia wa Iran katika kikao cha pande nne baina yao na Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA.
 
Katika ujumbe alioweka kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram, Mikhail Ulyanov ameandika: "katika kikao hicho, nchi hizo tatu ziliwasilisha waraka wa pamoja kwa Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kuhusiana na vipengele mbalimbali vya faili la nyuklia la Iran".
 
Wiki iliyopita, Grossi alifanya ziara mjini Tehran ambapo alikutana na na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Abbas Araghchi na Mohammad Eslami, Mkuu wa Shirika la Nishati ya Atomiki (AEOI). Katika mazungumzo hayo pande hizo mbili zilijadili mchakato wa ushirikiano wa kiufundi kati ya Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki.../