Chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa: Chombo cha Mauaji
Mauaji ya kudungwa kisu Muislamu nchini Ufaransa ndani ya Msikiti Khadija katika kijiji kilichoko kusini mwa nchi hiyo yameibua maswali mengi kuhusu kuongezeka mivutano ya kijamii na ubaguzi dhidi ya Waislamu, hasa ikitiliwa maanani kwamba chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu (Islamophobia) ni jambo linaloisumbua nchi ya Ufaransa
Ni baada ya Muislamu kuuawa nchini Ufaransa kwa kudungwa kisu takriban mara 50 na mwanamume Mfaransa mwenye chuki dhidi ya Uislamu ndani ya msikiti katika manispaa ya La Grand-Combe katika eneo la Le Gard kusini mashariki mwa Ufaransa.
Mfaransa Olivier H, 21, alimdunga kisu Aboubakar Cissé, 22, ndani ya Msikiti Khadija akitekeleza ibada ya Swala na kujirekodi akitekeleza uhalifu huo.
Jinai hii iliyolaaniwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, inaonyesha wazi athari za chuki dhidi ya Uislamu (Islamophobia), ambayo sasa imevuka mipaka ya matamshi ya chuki na ubaguzi, na kufikia kiwango cha kushambuliwa kimwili na hata mauaji dhidi ya Waislamu.
Hali hii inatoa taswira sahihi ya jinsi Waislamu nchini Ufaransa wanavyokabiliwa na mashinikizo ya kijamii ambayo yanawatia hofu na wasiwasi.

Vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kuchochea chuki dhidi ya Uislamu nchini Ufaransa, huku baadhi ya wadau wa vyombo hivyo wakisambaza zaidi maneno yanayochochea chuki dhidi ya Uislamu, jambo ambalo linatumiwa na makundi ya mrengo mkali wa kulia nchini Ufaransa.
Ufaransa ni mwenyeji wa mojawapo ya jumii kubwa zaidi za Waislamu barani Ulaya, na visa vya chuki dhidi ya Waislamu nchini humo vinatambuliwa kuwa vya juu zaidi.
Chuki dhidi ya Uislamu haikomei nchini Ufaransa. Kwa mujibu wa ripoti ya Wakala wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Ulaya, Waislamu barani humo kwa jumla wanakabiliwa na ongezeka la ubaguzi, ikibainisha kuwa ongezeko kubwa la chuki dhidi ya Waislamu limeshuhudiwa baada ya opesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa mnamo Oktoba 7, 2023, na hata kabla yake.
Kijana aliyeuawa siku ya Ijumaa anaitwa Aboubakar Cissé, mwenye asili ya Mali, na alikuwa amejitolea kila wiki kusafisha msikiti kabla ya Swala ya Ijumaa. Alikuwa peke yake wakati alipodungwa kisu na Olivier.