Iran yamwita balozi wa Uholanzi juu ya tuhuma 'zisizo na msingi' dhidi ya Tehran
Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imemwita balozi wa Uholanzi kuwasilisha malalamiko makali ya Tehran dhidi ya tuhuma "zisizo na msingi" zilizotolewa na Uholanzi dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Emiel de Bont aliitwa katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Ulaya Magharibi, Alireza Yousefi jana Ijumaa kukabidhiwa malalamiko ya Iran.
Katika mkutano huo, Yousefi alipinga madai dhidi ya Iran yaliyotolewa na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Uholanzi na kumwita balozi wa Iran katika Wizara ya Mambo ya Nje ya nchi hiyo ya Ulaya.
"Inasikitisha kwamba chombo cha kidiplomasia cha Uholanzi kinatoa tu tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Iran kwa msingi wa 'dhahania' na 'tuhuma' zilizoibuliwa na taasisi za usalama za nchi hiyo na utawala wa Kizayuni, na baadaye kumwita balozi wa Iran juu ya uwongo huu wa kipuuzi," amesema.
Hatua ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi ni mchezo wa lawama wa "wazi na usiokubalika", amebainisha Yousefi, akisema upande unaopaswa kuwajibishwa kwa kuwahifadhi wahalifu na magaidi hauna haki ya kimaadili ya kuwatuhumu wengine.
Yousefi pia ametoa wito kwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi kuwa na mchango athirifu katika maendeleo ya Asia Magharibi, kwa kufuata mtazamo wa kitaalamu na wa heshima katika uhusiano wa pande mbili na Iran, kujiepusha kukariri madai ya uwongo na yasiyo na msingi, na kusitisha uungaji mkono wake wa kila upande kwa utawala wa Kizayuni wa Israel unaofanya mauaji ya kimbari.
Balozi wa Uholanzi, kwa upande wake, amesema atafikisha malalamiko ya Tehran kwa serikali yake.Siku ya Alkhamisi, Idara ya Ujasusi na Usalama ya Uholanzi, inayojulikana kama AIVD, ilidai katika ripoti yake ya kila mwaka kwamba, Iran imehusika na majaribio mawili ya mauaji huko barani Ulaya. Tuhuma hizo zilipelekea Wizara ya Mambo ya Nje ya Uholanzi kumwita balozi wa Iran.